Jumanne, Novemba 24, 2026
HABARI MPYA
Kitaifa

NGOs 3,500 KUKUTANA DODOMA, MBIO ZA HISANI KUANZISHA MFUKO WA RUZUKU

DODOMA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa washiriki takribani 3,500 kutoka ndani na nje ya sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), watakaokutana katika Jukwaa la Sita la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, litakalofanyika Novemba 25 hadi 28, mwaka huu, huku mbio za hisani zikitarajiwa kuchangisha fedha za kuanzisha mfuko wa pamoja wa ruzuku kwa mashirika hayo.
Mbio hizo ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha uendelevu wa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini, kwa kupunguza utegemezi wa ufadhili kutoka nje na kuongeza uwezo wa kupata rasilimali fedha kupitia vyanzo vya ndani.
Jukwaa hilo limeandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), likiwa na lengo la kujadili namna ya kuimarisha sekta hiyo kupitia ubunifu, ubia na upatikanaji wa rasilimali fedha za ndani.
Akizungumza na waandishi wa habari Leo November 23,2026 jijini Dodoma kuhusu maandalizi ya jukwaa hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni “Fikra Mpya kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha kupitia Vyanzo vya Ndani.”
Amesema kaulimbiu hiyo imezingatia changamoto zinazoikabili sekta hiyo, ikiwamo utegemezi mkubwa wa ufadhili, masharti magumu ya wafadhili na kutotabirika kwa upatikanaji wa fedha, hali inayofanya mashirika hayo kuwa na changamoto katika kutekeleza shughuli zake kwa uendelevu.
“Mwelekeo mpya ni kuhakikisha tunatumia rasilimali za ndani ya nchi yetu ili kuimarisha uwezo wa mashirika haya na kuyafanya yaweze kuendelea kutoa huduma kwa wananchi bila kutegemea zaidi ufadhili wa nje,” amesema.
Amesema mgeni rasmi katika jukwaa hilo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba.
Washiriki wanaotarajiwa kuhudhuria ni pamoja na wawakilishi wa wizara, idara za Serikali, taasisi za kisekta, sekretarieti za mikoa, mamlaka za Serikali za Mitaa, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, vyombo vya habari, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wanufaika wa miradi inayotekelezwa na mashirika hayo na jamii kwa ujumla.
Katika kuunga mkono juhudi za kuimarisha sekta hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kutakuwa na mbio za hisani za mashirika yasiyo ya kiserikali zitakazofanyika Jumamosi, Novemba 28, mwaka huu, jijini Dodoma.
Amesema mbio hizo zitaanzia na kuhitimishwa katika Uwanja wa Jamhuri, kuanzia saa 11:30 alfajiri hadi saa 1:30 asubuhi, huku washiriki wakipita katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na Stesheni ya Reli ya Kisasa ya SGR ya Samia Suluhu Hassan.
Ameeleza kuwa lengo kuu la mbio hizo ni kukusanya fedha zitakazotumika kama kianzio cha Mfuko wa Pamoja wa Ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs Basket Fund – NBF), ambao unalenga kupunguza utegemezi wa ufadhili na kuimarisha uwezo wa kifedha wa mashirika yanayotoa huduma mbalimbali kwa wananchi, hususan katika ngazi ya jamii.
Amesema mbio hizo si shughuli ya michezo pekee, bali ni jukwaa la wadau na wananchi kushiriki moja kwa moja katika kuchangia ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa.
Ameongeza kuwa wananchi ambao hawataweza kushiriki kwa kukimbia wana nafasi ya kuchangia fedha au vifaa ili kusaidia kuanzishwa na kuimarishwa kwa mfuko huo.
“Hii ni hatua ya kudumu ya kuoanisha sekta hii na safari ya maendeleo ya taifa, kwa sababu sekta imara ya mashirika yasiyo ya kiserikali inamaanisha familia imara, jamii imara na taifa imara,” amesema.
Aidha, amesema kuanzishwa kwa mfuko huo kutasaidia mashirika yasiyo ya kiserikali kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuendeleza miradi na huduma za kijamii kwa muda mrefu, badala ya kutegemea misaada ambayo wakati mwingine huwa haipatikani kwa uhakika.
Akizungumzia umuhimu wa Dodoma kuwa mwenyeji wa jukwaa hilo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema anafurahia heshima hiyo, akieleza kuwa ni fursa ya kuendelea kuitangaza Dodoma kama kitovu cha mikutano mikubwa ya kitaifa, maonyesho na shughuli zinazolenga kuwaletea wananchi maendeleo.
Amesema tukio hilo pia linatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi kwa kuongeza wateja katika hoteli, huduma za usafiri na usafirishaji pamoja na biashara na huduma nyingine za kijamii.
Kutokana na umuhimu wa jukwaa hilo, amevitaka vyombo vya habari kushirikiana na Serikali kuhamasisha wananchi wa Dodoma na wadau kutoka maeneo mbalimbali nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli zote zilizopangwa ili kuhakikisha linafanikiwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa.