Mshauri wa Rais wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Ummy Mwalimu, ametoa wito kwa vijana na wanawake kushirikishwa kikamilifu katika maamuzi na mipango ya kuboresha huduma za afya badala ya kuishia kuwasikiliza na kuwapa ahadi.
Akizungumza katika Mkutano wa Afya na Uzazi kwa Vijana jijini Addis Ababa, Ethiopia, Ummy amesema Serikali na wadau wanapaswa kuelekeza nguvu katika kugharamia na kuhakikisha huduma za afya zinawafikia vijana, wanawake na watoto.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Mstaafu wa Uganda, Dkt. Speciosa Wandira Kazibwe, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha kinga na kushughulikia sababu za msingi za magonjwa ili kupunguza magonjwa na vifo vinavyoweza kuzuilika.
Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), Dkt. Ntuli Kapologwe, pamoja na Josephat Rafael na Rahma Suleiman Jumanne, ni miongoni mwa washiriki kutoka Tanzania waliopongeza jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, katika kuendeleza ajenda hiyo barani Afrika.




