Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Mabalozi wa Ufaransa, Misri na Afrika Kusini wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania, leo tarehe 23 Novemba 2026, Ikulu Zanzibar.

Mabalozi wa Ufaransa na Misri wamefika Ikulu Zanzibar kujitambulisha rasmi baada ya kuanza majukumu yao, huku Balozi wa Afrika Kusini akifika kuaga baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini.

Katika mazungumzo na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mhe. Dkt. Jean-Baptiste Jeangène Vilmer, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inaendelea kuangalia namna ya kushirikiana na taasisi ya mafunzo ya hoteli na utalii ya Ufaransa katika kuwajengea vijana ujuzi wa vitendo unaohitajika katika sekta hiyo.

Amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha vijana kupata ujuzi na sifa zinazotambulika kimataifa ili kuongeza nafasi za kupata ajira katika hoteli na kujiendeleza hadi kufikia nafasi za usimamizi.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inaendelea kuvutia uwekezaji mkubwa katika sekta ya utalii, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko, hususan katika huduma za hoteli, migahawa, mapokezi na usimamizi.

Aidha, amezikaribisha kampuni za Ufaransa kuwekeza katika utalii wa mikutano na michezo, uvuvi, ufugaji wa samaki, usarifu wa mwani na nishati mbadala, akieleza kuwa Zanzibar ina fursa kubwa katika Uchumi wa Buluu zinazoweza kuendelezwa kupitia uwekezaji, teknolojia na utaalamu.

Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa Zanzibar kuongeza uwezo wake wa uzalishaji wa nishati ya umeme ili kukidhi mahitaji yanayoendelea kuongezeka, kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa umeme na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nje. Katika hilo, Rais Dkt. Mwinyi amezikaribisha kampuni na wawekezaji kutoka Ufaransa kuangalia fursa zilizopo katika nishati mbadala, hatua itakayosaidia kuimarisha shughuli za uzalishaji, uwekezaji na ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake, Balozi Jeangène Vilmer amesema Ufaransa iko tayari kuendeleza ushirikiano na Zanzibar katika maeneo ya utalii, uwekezaji, elimu, utamaduni na maendeleo, akieleza kuwa sekta binafsi na taasisi za Ufaransa zina nafasi ya kushiriki zaidi katika fursa zinazopatikana Zanzibar.

Katika mazungumzo na Balozi wa Misri nchini Tanzania, Mhe. Rania Abdel-Meguid, Rais Dkt. Mwinyi ameiomba Serikali ya Misri kuangalia uwezekano wa kuanzisha ziara za mara kwa mara za madaktari bingwa wa moyo Zanzibar, ili kutoa huduma kwa wagonjwa na wakati huo huo kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa Zanzibar.

Amesema Zanzibar tayari imewekeza katika matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo, ikiwemo kuanzishwa kwa huduma ya Catheterisation (CATH-LAB) katika Hospitali ya Lumumba. Hata hivyo, bado kuna upungufu wa wataalamu wa kutosha kutoa huduma hizo kwa ufanisi.

Rais Dkt. Mwinyi pia ameunga mkono wazo la kuimarisha ushirikiano wa utalii kati ya Zanzibar na Sharm el-Sheikh, ikiwemo kubadilishana uzoefu katika huduma za wageni na kuandaa vifurushi vya utalii vinavyoweza kuwaunganisha watalii wanaotembelea Misri, Zanzibar na mbuga za wanyama Tanzania Bara

Rais Dkt. Mwinyi pia amepongeza uwekezaji wa kampuni za Misri uliopo Zanzibar na kueleza kuwa bado kuna fursa zaidi za ushirikiano katika utalii, miundombinu, nishati, kilimo na sekta nyingine za maendeleo.

Pia amesisitiza haja ya kuimarisha uratibu katika miradi ya kilimo inayoshirikisha taasisi za Zanzibar na kampuni za Misri ili miradi hiyo iweze kutekelezwa kwa ufanisi na kutoa matokeo yaliyokusudiwa.

Balozi Rania ameonesha utayari wa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika maeneo hayo, ikiwemo afya, utalii, miundombinu, nishati na kilimo.

Kwa upande wa Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Mhe. Noluthando Mayende-Malepe, Rais Dkt. Mwinyi amemshukuru kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini katika kipindi cha utumishi wake.

Rais Dkt. Mwinyi pia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuhifadhi historia ya pamoja ya mapambano ya ukombozi kati ya Tanzania na Afrika Kusini, ikiwemo kuendeleza eneo la kumbukumbu ili historia hiyo iendelee kufahamika na kuthaminiwa na vizazi vijavyo.

Aidha, mazungumzo yao yamegusa fursa za kuimarisha ushirikiano katika utalii na uwekezaji, hususan katika maeneo ya Uchumi wa Buluu.

Rais Dkt. Mwinyi amemtakia Mhe. Mayende-Malepe mafanikio katika majukumu yake yajayo na kumhakikishia kuwa Zanzibar itaendelea kumkaribisha na kuthamini mchango wake katika kuimarisha uhusiano baina ya pande hizo.