Na Mwandishi Wetu
BOLT Tanzania imewahimiza abiria kuripoti matukio yanayohatarisha usalama moja kwa moja kupitia programu yake, ikionya kuwa kutegemea malalamiko kwenye mitandao ya kijamii pekee kunaweza kuchelewesha utambuzi wa safari husika na hatua za kushughulikia tukio.
Ujumbe huo ulitolewa katika warsha ya uhamasishaji kuhusu usalama iliyoandaliwa kwa kushirikiana na Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Warsha hiyo iliwakutanisha wanafunzi zaidi ya 300 pamoja na wawakilishi wa Bolt, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) na chuo hicho.
Changamoto ni kwamba malalamiko yanayochapishwa kwenye mitandao ya kijamii yanaweza kukosa taarifa za agizo la safari zinazohitajika kumtambua abiria, dereva na safari husika. Kupata taarifa hizo kunaweza kuhitaji ufuatiliaji wa ziada kabla ya uchunguzi wa malalamiko kuanza.
Kuripoti kupitia programu kunawapa watumiaji njia ya moja kwa moja ya kueleza kilichotokea na kubainisha safari inayohusika. Kwa mujibu wa taarifa ya Bolt kuhusu faragha ya watumiaji nchini Tanzania, timu zake za usaidizi na usalama hutumia taarifa zinazotolewa na watumiaji kuchunguza malalamiko ya usalama na madai ya vitendo vya uhalifu.
Meneja wa Uendeshaji wa Bolt Tanzania, Ludwigy Bwana, alisema ushirikiano huo na chuo ulilenga kuziba mapengo ya uelewa wa watumiaji kuhusu usalama.
“Wanafunzi ni sehemu muhimu ya watumiaji wa Bolt, na ushirikiano huu unasaidia kuziba mapengo ya uelewa katika maeneo muhimu kama usalama,” alisema.
“Vipengele vya usalama huwa na manufaa zaidi pale watu wanapojua kuvitumia.”
Wanafunzi walijifunza kuhusu vipengele vinane vya usalama vinavyopatikana Tanzania, vikiwemo namba maalumu za uthibitisho wa safari (Pickup Codes), uthibitishaji wa utambulisho wa dereva kwa picha ya uso, kushirikisha wengine taarifa za safari na kipengele cha ufuatiliaji wa safari cha Ride Check.
Maonesho ya vitendo yalihusisha matumizi ya vipengele hivyo katika mazingira ya kila siku, kuanzia kuhakikisha dereva aliyefika ndiye aliyeoneshwa kwenye programu hadi kuwashirikisha wanafamilia taarifa za safari.
Warsha hiyo pia ilisisitiza wajibu wa abiria kuripoti vitendo vinavyohatarisha usalama na kudai huduma za usafiri zinazozingatia sheria na kanuni.
“Abiria wana haki na wajibu wa kudai huduma zinazokidhi matakwa ya kisheria,” alisema Pateli Ngereza, Kaimu Meneja wa Udhibiti wa Magari ya Usafiri wa Abiria na Mkuu wa LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.
Aliwahimiza wanafunzi kutumia mifumo iliyopo ya uhakiki, ikiwemo programu ya LATRA, kuchagua vyombo vya usafiri vyenye leseni na kutumia kofia ngumu au mikanda ya usalama.
Kutoa malalamiko hadharani kunaendelea kuwa njia ya kuibua hoja na kudai uwajibikaji. Kuripoti moja kwa moja huwezesha watumiaji kuwasiliana mara moja na huduma kwa wateja, malalamiko kufuatiliwa kwa wakati, kupatikana kwa taarifa za uchunguzi na kampuni kuchukua hatua zinazofaa.
Kwa watu walio katika hatari ya haraka au waliojeruhiwa, kuripoti kupitia programu kunapaswa kwenda sambamba na kuwasiliana haraka na polisi au huduma za dharura, kulingana na hali ilivyo. Mwongozo uliochapishwa na Bolt unawashauri watumiaji kutafuta msaada wa dharura inapohitajika na pia kuitaarifu timu yake ya usaidizi.



