Na Mwandishi wetu-Kibaha
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Pwani kwa utendaji kazi wao sambamba na kutatua changamoto za walipa kodi.
Jumaa ameyasema hayo katika ziara ya siku moja ya Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, ambapo ulifanyika mkutano wa hadhara uliowakutanisha wakazi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha.
Akizungumza katika mkutano huo Mbunge huyo amesema, yapo maboresho ya huduma yamefanywa na Mamlaka hiyo ambayo yamejenga mahusiano mazuri na wananchi na kuwafanya kuwa na mwamko wa kulipa kodi bila usumbufu.
“Niwapongeze TRA kwa huduma zao kwa wananchi, wanafanya kazi vizuri na kujenga mahusiano kwa walipa kodi na hii ni moja ya kitu ambacho kitaongeza makusanyo na miradi kutekelezwa kwa wakati,” amesema.
Amesema kwasasa hakuna tena biashara zinazofungwa, elimu ya kodi imekuwa sababu ya kuchochea mahusiano mazuri huku akieleza kwamba wafanyabiashara wenye changamoto zinatatuliwa bila kikwazo.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo ameiomba Serikali kusaidia ujenzi wa uzio katika Hospitali ya Wilaya, sambamba na ujenzi wa barabara ya Mlandizi Manerumango kwa kiwango cha lami.
Baadhi ta Wananchi walioshiriki mkutano kumsikiliza Waziri Mkuu Issa Mohamed na Juliius Santos waliomba ziara ya kiongozi huyo kufanyika mara kwa mara kwani inasaidia wananchi kutatuliwa changamoto zao.


