Jumanne, Novemba 24, 2026
HABARI MPYA
Kitaifa

WAZIRI MKUU ATAKA UJENZI WA SHULE YA MISEGESE UKAMILIKE JANUARI 31

 

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi kuhakikisha ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Misegese, mkoani Morogoro, unakamilika ifikapo Januari 31, 2027, ili kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali wa kilometa 11 hadi 15 kwenda shule.

Ametoa maelekezo hayo leo, Jumanne, Novemba 24, 2026, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Toboatobo, wilayani Malinyi, baada ya kumhoji Mkurugenzi huyo kuhusu muda wa kukamilisha ujenzi wa shule hiyo.

Akijibu swali la Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Christopher Aloyce Sanga, amesema ujenzi utakamilika Januari 31, 2027, tarehe ambayo Dkt. Mwigulu ameikubali na kusisitiza shule ikamilike ili wanafunzi waanze masomo.

Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro, ambapo pia amekagua maendeleo ya ujenzi na kuweka jiwe la msingi la shule hiyo iliyopo Kijiji cha Misegese, Kata ya Malinyi.

Dkt. Mwigulu amesisitiza matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa na Serikali, akionya dhidi ya visingizio vya upungufu wa fedha na kuwataka wasimamizi wa mradi kutowasumbua wananchi katika utekelezaji wake.

“Na sitaki kusikia pesa imepungua,” amesema Waziri Mkuu, akisisitiza kuwa fedha zilizotolewa zinapaswa kutumika kukamilisha mradi huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa mradi iliyowasilishwa kwa Waziri Mkuu, Serikali imetoa Sh. milioni 528.9 kupitia Mradi wa Kuboresha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo, ambao umefikia takribani asilimia 60.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mradi unahusisha ujenzi wa madarasa manane, ofisi mbili za walimu, jengo la utawala, maktaba, jengo la TEHAMA, maabara tatu za sayansi, vyoo na tenki la maji.

Shule hiyo itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 320, huku ikitarajiwa kuanza kwa kupokea wanafunzi 80 wa kidato cha kwanza.

Kukamilika kwa shule hiyo kutapunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali wa kilometa 11 hadi 15 kwenda kupata elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Malinyi.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu pia amepanda mti wa mkongo katika eneo la shule ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira.