SHIRIKISHO la Soka Barani Afrika (CAF), limemteua mwamuzi raia wa Tanzania, Ahmed Arajiga kuchezesha mechi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika itakayoikutanisha USM Alger ya Algeria dhidi ya AS Real de Bamako ya Mali.
Mechi hiyo ya kundi D, itakayopigwa Novemba 29, 2026, Stade du 5 Juillet, mjini, Algiers, Algeria, Arajiga mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), amekabidhiwa jukumu hilo na kuzidi kuipeperusha vizuri bendera ya Tanzania.
Arajiga mwenye uzoefu mkubwa baada ya kuchezesha hivi karibuni mechi ya Kariakoo Derby ambayo Simba ilishinda mabao 2-1, dhidi ya Yanga, kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini, Dar es Salaam, Oktoba 10, 2026, ameendelea kung’ara upande wa kimataifa.
Katika mechi hiyo ya Novemba 29, 2026, Arajiga atasimamia kati, huku kwa upande wa Video Assistant Referee yaani (VAR), Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), limemteua mwamuzi kutoka Zimbabwe, Brighton Chimene kusimamia teknolojia hiyo.
Arajiga mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ni miongoni mwa waamuzi 35, walioteuliwa na CAF kwa lengo la kupata mafunzo mazuri ya kujiandaa na mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.


