WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe,akizungumza katika Mkutano wa 10 wa Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka 2025/2026 leo Novemba 24,2026 jijini Dodoma,
Na.Alex Sonna,MZALENDO BLOG-DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amezitaka halmashauri nchini kuimarisha utekelezaji wa afua za lishe kwa kushirikisha sekta mbalimbali, ili kukabiliana na changamoto za lishe zinazoweza kudhoofisha afya ya wananchi na kasi ya maendeleo ya taifa.
Aidha, amezitaka halmashauri ambazo hazijafanya vizuri katika utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kuongeza juhudi, huku zile zilizopiga hatua ziendelea kuimarisha utendaji wake ili kufikia viwango vinavyotarajiwa.
Akizungumza katika Mkutano wa 10 wa Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka 2025/2026 jijini Dodoma,Prof. Shemdoe amesema lishe bora ni msingi wa kujenga rasilimali watu wenye afya na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.
Amesema changamoto za lishe zinaathiri maendeleo katika ngazi ya kaya, jamii, halmashauri, mikoa na taifa kwa ujumla, hivyo zinahitaji juhudi za pamoja kutoka sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, afya, elimu, maji, hifadhi ya jamii na usafi wa mazingira.
“Uboreshaji wa hali ya lishe ya jamii ni jukumu la pamoja na unahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali. Kila sekta ina mchango wake katika kuhakikisha tunakabiliana na matatizo ya lishe nchini,” amesema Prof. Shemdoe

Amesema tathmini ya utekelezaji wa mkataba huo imeonesha mafanikio katika maeneo mbalimbali, ikiwemo uhamasishaji na upatikanaji wa fedha za kutekeleza afua za lishe, ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026 lengo lilikuwa kukusanya na kuelekeza Sh bilioni 207.2, huku halmashauri zikiweza kufikisha Sh bilioni 70.8.
Prof. Shemdoe amewapongeza viongozi wa mikoa na halmashauri kwa juhudi zilizofanyika, akiwataka kuendelea kusimamia upatikanaji wa fedha na kuhakikisha zinatumika kutekeleza mipango ya lishe katika maeneo yao.
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuanza kwa tafiti za kiutendaji kuhusu lishe katika mikoa ya Mtwara, Njombe na Iringa, pamoja na baadhi ya halmashauri zilizotumia mapato ya ndani kugharamia tafiti hizo.
Aidha Prof. Shemdoe amezihimiza halmashauri ambazo bado hazijafanya tafiti hizo kutenga fedha ili kupata taarifa zitakazosaidia kubaini changamoto na kuweka mikakati inayozingatia mahitaji halisi ya wananchi.

Katika hatua nyingine,amesema juhudi zimefanyika kuimarisha upatikanaji wa vyakula vilivyoongezwa virutubisho, hususan katika shule, huku akisisitiza hatua hiyo iendelee ili jamii ipate chakula chenye ubora na virutubisho vinavyohitajika.
Kuhusu ushiriki wa viongozi katika utekelezaji wa afua za lishe, amesema wakuu wa mikoa na wilaya wamekuwa mstari wa mbele katika ufuatiliaji na uhamasishaji wa jamii, huku watendaji wa kata na vijiji wakiendelea kutekeleza afua hizo katika maeneo yao.
Aidha, amewapongeza viongozi wa mikoa na halmashauri kwa mafanikio yaliyopatikana katika matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato, akibainisha kuwa kiwango cha halmashauri zilizofunga mifumo hiyo kimeongezeka kutoka asilimia nane mwaka uliopita hadi asilimia 92 katika mwaka wa tathmini.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza mapato ya halmashauri na kuwezesha upatikanaji wa fedha za kuboresha huduma za jamii, ikiwemo ununuzi wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Ameeleza kuwa uwezo wa ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka chini ya Sh bilioni moja kwa wiki katika kipindi kilichopita hadi kati ya Sh bilioni 3.2 na Sh bilioni 3.6 kwa wiki kwa sasa.
Hata hivyo, amewataka viongozi kuhakikisha mifumo yote iliyofungwa inatumika ipasavyo na halmashauri zilizobaki kukamilisha hatua hiyo ili kufikia asilimia 100.
Prof. Shemdoe pia amewapongeza mikoa iliyofanya vizuri na ile iliyoonesha maboresho, akitolea mfano Mkoa wa Simiyu ambao, kwa mujibu wa maelezo yake, uliwahi kutajwa katika kundi la mikoa iliyokuwa na changamoto lakini umeonesha maendeleo katika tathmini ya mwaka huu.
“Mkataba wa lishe ulioanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, umeimarisha mifumo ya usimamizi wa lishe katika mikoa na halmashauri nchini na kuchochea juhudi za kuboresha afya ya wananchi.”amesema
Prof. Shemdoe,amegusia mkakati wa Afrika wa afya ya mama na mtoto unaolenga kufikia sifuri tatu, ambazo ni kuondoa wanawake wanaojifungulia majumbani, kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo.
Amesema Tanzania inaendelea kushiriki katika utekelezaji wa mkakati huo, akiwapongeza viongozi na watendaji wanaosimamia huduma za afya ya mama na mtoto.
Amewahimiza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na watendaji wengine kuendelea kusikiliza wananchi, kutatua migogoro na kutekeleza majukumu yao kwa bidii ili kuboresha huduma na kuleta maendeleo katika maeneo yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, Florent Kyombo,amezitaka halmashauri nchini kuongeza bajeti ya lishe katika maandalizi ya bajeti ya mwaka 2027, akisisitiza kuwa fedha zinazotengwa zinapaswa kuzidi kiwango cha chini cha Sh1,000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano ili kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za lishe.
Kyombo amesema uwekezaji wa kutosha katika lishe ni muhimu katika kupunguza changamoto za utapiamlo na kuboresha afya na ukuaji wa watoto, huku akizitaka halmashauri kutumia mapato yake ya ndani kutenga fedha zinazokidhi mahitaji halisi ya utekelezaji wa afua za lishe.
Amesema Mwongozo wa Uandaaji na Utekelezaji wa Bajeti unazitaka halmashauri kutenga kiasi kisichopungua Sh1,000 kwa kila mtoto aliye chini ya miaka mitano.
Amesema kiwango hicho ni kiwango cha chini kinachotakiwa, hivyo halmashauri zinapaswa kufanya tathmini ya mahitaji yake na kutenga fedha zaidi kulingana na uwezo na vipaumbele vya maeneo yao.
“Naomba niwasisitize kuwa mwongozo umesema zisizopungua Sh1,000 kwa kila mtoto. Tunataka kuona halmashauri zetu zinajipima na kusema badala ya Sh1,000, sisi tumetenga Sh1,200, Sh1,500 au Sh2,000,” amesema Kyombo.
amesema Kamati ya Bunge itaendelea kushirikiana na Wizara pamoja na kusimamia na kuishauri Serikali katika kuhakikisha huduma za lishe zinaboreshwa kwa ustawi wa wananchi.
Ameeleza kuwa mikutano ya tathmini ni muhimu kwa kuwa inatoa fursa ya kubaini changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa afua za lishe, kutambua mafanikio yaliyopatikana na kuweka mikakati mipya ya kuboresha utendaji katika ngazi zote.
“Lishe inahitaji dhamira ya kweli, uwajibikaji na usimamizi wa karibu kuhakikisha kila mtoto anapata lishe bora. Tukiwa na bajeti ya kutosha na usimamizi mzuri, tutaona mabadiliko makubwa katika viashiria vya lishe,” amesema.
Naye Mwakilishi wa Katibu Wizara ya Afya ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dkt. Ahmad Mohamed Makuwani, amesema kuwa wameimarisha mikakati ya kukabiliana na changamoto za utapiamlo nchini kwa kuongeza wataalamu wa lishe, kusambaza mashine 300 za kuongeza virutubisho kwenye vyakula na kuimarisha huduma za lishe katika ngazi ya jamii.
Hatua hizo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha afya na maendeleo ya watoto, wajawazito na wananchi kwa ujumla, huku ikisisitiza kuwa lishe bora ni msingi wa ukuaji wa binadamu kiakili na kimwili pamoja na kuongeza tija katika uzalishaji na maendeleo ya taifa.
Amesema Wizara inaendelea kutekeleza afua mbalimbali kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI na wadau wa lishe ili kukabiliana na utapiamlo wa aina mbalimbali.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, Wizara ilinunua mashine 300 za kuongeza virutubisho maarufu kama Dosifier na kuzisambaza kwa wasindikaji wadogo na wa kati katika mikoa mbalimbali ili kuimarisha urutubishaji wa unga wa ngano na mahindi.
Aidha, amesema “Wizara imenunua mashine 12 za maabara zinazojulikana kama iCheck na kuzisambaza katika mikoa 12 kwa ajili ya kuimarisha uhakiki wa vyakula vinavyorutubishwa, akiwahakikishia wananchi kuwa virutubisho hivyo vimepitia taratibu za uhakiki na ni salama kwa matumizi.”amesema Dkt. Makuwani
Awali MKuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi.Rosemary Senyamule,amesema licha ya hatua zilizofikiwa, mkoa unaendelea kupambana na changamoto zilizopo kwa kuweka mikakati madhubuti na kuongeza ushirikiano na wadau wenye utaalamu katika sekta ya lishe.
Amebainisha kuwa UDOM ni miongoni mwa wadau muhimu wanaoshirikiana na mkoa huo, ambapo kupitia kitengo chake cha lishe wamekubali kufanya utafiti katika wilaya zote za Dodoma ili kupata takwimu za sasa zitakazosaidia kupanga na kutekeleza afua zinazolenga kuboresha lishe ya wananchi.
Amesema utafiti huo tayari umeanza katika Wilaya za Chamwino na Dodoma, akieleza kuwa matokeo yake yatakapokamilika yatawasilishwa kwa viongozi wa kitaifa ili kutoa picha halisi ya hali ya lishe katika mkoa huo na kusaidia kubaini maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele.
“UDOM wamekuwa washauri wazuri kwetu, wamekubali kutumia utaalamu wao kufanya utafiti katika wilaya zote za mkoa wa Dodoma ili tujue hali halisi ya lishe kwa sasa. Tunawashukuru kwa kuwa sehemu ya juhudi zetu za kuboresha lishe,” amesema Senyamule.


