Katika kikao hicho, wajumbe walijadili masuala mbalimbali yanayohusu uthabiti wa sekta ya fedha, yakiwemo Ripoti ya Uthabiti wa Sekta ya Fedha kwa nusu mwaka unaoishia Juni 2026, Mwongozo wa Zoezi la Uigaji wa Migogoro ya Kifedha pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Ufadhili wa Miradi ya Kaboni wa mwaka 2026-2031.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Tutuba alisema kuwa Tanzania imepiga hatua katika kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha kutokana na ushirikiano na uratibu mzuri miongoni mwa mamlaka za udhibiti na usimamizi wa sekta hiyo.
Alibainisha kuwa mafanikio hayo yanajumuisha kuendelea kwa uchumi kuwa stahimilivu dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kuathiri sekta ya fedha, pamoja na utekelezaji wa mikakati ya kupambana na Utakatishaji Fedha Haramu, Ufadhili wa Ugaidi na Ufadhili wa Silaha za Maangamizi (AML/CFT).
Aidha, Jukwaa liliridhia na kuidhinisha Mkakati wa Kitaifa wa Ufadhili wa Miradi ya Kaboni wa mwaka 2026–2031, unaolenga kuongeza upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya kaboni na kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika masoko ya kaboni ya kikanda na kimataifa.
Jukwaa hilo linajumuisha taasisi 15 za udhibiti na usimamizi wa sekta ya fedha, zikiwemo Benki Kuu ya Tanzania, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Fedha, Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) na Bodi ya Bima ya Amana (DIB).






