Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewakutanisha wadau wa gesi asilia iliyokandamizwa (CNG), wakiwemo watoa huduma na watumiaji, katika semina inayolenga kuongeza uelewa kuhusu usalama, ubora na ufanisi wa huduma za gesi asilia nchini.
Semina hiyo imefunguliwa na Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki, Mhandisi Lorivii Long’idu, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Bw. Salum Mnuna.
Semina hiyo ilihudhuriwa na wadau kutoka Wizara ya Nishati, wamiliki na waendesha vituo vya CNG, wataalamu wa ukaguzi na ufungaji wa mifumo ya gesi kwenye magari, UDSM, DIT, TBS, TPDC, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Bodi ya Wakandarasi Tanzania, EWURA CCC, CRDB Bank pamoja na wadau wengine wa sekta hiyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mhandisi Long’idu amesisitiza umuhimu wa wadau kuzingatia viwango na taratibu za usalama katika shughuli zote za CNG ili kulinda maisha, mali na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ubora unaotakiwa.
Aidha, ameeleza kuwa EWURA inafanya mapitio ya viwango vya bei kikomo na faida kwa watoa huduma za CNG, baada ya takribani miaka 15 bila mabadiliko, ili kuzingatia mabadiliko ya gharama za uwekezaji na uendeshaji. Mapendekezo hayo yanatarajiwa kuanza kutumika Desemba 2026.
Amewahimiza wadau kutoa maoni kuhusu mapendekezo hayo ili kuhakikisha maamuzi yatakayofikiwa yanazingatia maslahi ya watoa huduma na watumiaji, gharama halisi za uendeshaji pamoja na uwezo wa wananchi kumudu huduma hizo.
Ameongeza kuwa EWURA itaendelea kushirikiana na wadau katika kuhakikisha sekta ya gesi asilia inakua kwa kuzingatia usalama, ubora, uwajibikaji na uendelevu wa huduma kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.



