Uncategorized

REA KUENDELEA KUWEZESHA SEKTA BINAFSI KUSHIRIKI KATIKA UZALISHAJI UMEME

Written by Alex Sonna

 

📍MAGU, MWANZA.

Bodi ya Nishati Vijijini (REB) imeeleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi wa ndogo wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia mfumo wa umeme jua unaochangia Megawati Tano katika Gridi ya Taifa.

Akizungumza leo Novemba 19, 2026 wakati wa ziara ya kutembelea mradi huo katika Kijiji cha Bugando Wilayani Magu Mkoani Mwanza, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini REB, Mhe. Balozi Radhia Msuya amesema kukamilika kwa mradi huo ni hatua muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Wilaya ya Magu na Taifa kwa ujumla, huku akiahidi kuwa, REA itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendeleza miradi ya kuzalisha umeme kwa njia mbalimbali inayobuniwa na kutekelezwa na waendelezaji wadogo.

Amesema mradi huo una mchango mkubwa katika kuunga mkono juhudi za wananchi wa Magu za kujenga uchumi wa viwanda kupitia upatikanaji wa umeme wa uhakika.

“Ni furaha kuona mradi huu umekamilika na sasa unaendelea kuunga mkono juhudi za wananchi wa Magu za kujenga uchumi wa viwanda,” amesema Balozi Msuya.

Aidha Balozi Msuya amesema matarajio ya Bodi ni kuona mradi huo unaongeza uwezo wake wa uzalishaji ili kuchangia zaidi katika upatikanaji wa umeme nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Amina Makilagi ameishukuru Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo ambao umeongeza upatikanaji wa umeme na kuunga mkono utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya wilaya hiyo.

Amesema Wilaya ya Magu imejipanga kukuza uwekezaji katika sekta za viwanda, kilimo na ufugaji hivyo upatikanaji wa umeme ni kichocheo muhimu katika kufanikisha malengo hayo.

Aidha Mhe. Makilagi ameahidi kuhakikisha mradi huo unalindwa na kuendelezwa ili uendelee kutoa mchango wake katika Gridi ya Taifa na kuongeza upatikanaji wa umeme.

“Ninachoweza kusema ni kwamba mradi huu tutaulinda na kuhakikisha unakuwa salama na endelevu ili uendelee kuleta matokeo chanya kwa wananchi,” amesema Makilagi.

Vilevile ameishukuru REA kwa kuendelea na juhudi za kuhakikisha vitongoji vyote nchini vinapata huduma ya umeme.

Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Bugando Natural Energy, ambao ndio wawekezaji wa mradi huo, Joseph Jirabi ameishukuru REA kwa kuwezesha kukamilika kwa mradi huo ambao kwa sasa unachangia megawati tano za umeme katika Gridi ya Taifa.

Jirabi amesema kuwa katika mipango ya baadaye mradi huo unalenga kuongeza uzalishaji hadi kufikia megawati 10 ili kuendelea kuchangia katika kuboresha upatikanaji wa umeme kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

About the author

Alex Sonna