Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb.), tarehe 12 Oktoba 2026, amezindua mradi wa kiwanda cha kuzalisha kokoto katika eneo la Nanja, Wilaya ya Monduli, Mkoa wa Arusha. Mradi huo unatekelezwa na Shirika la Mzinga, linalomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ukiwa na lengo la kupanua wigo wa shughuli za kiuchumi za Shirika na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Waziri Nyansaho amesema kuwa mradi huo ni uwekezaji wa kimkakati unaoendana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii, pamoja na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Ameeleza kuwa uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Shirika la Mzinga ya kuimarisha shughuli zake za uzalishaji, kuongeza vyanzo vya mapato na kutumia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali za uchumi kwa manufaa ya Shirika, Jeshi na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Nyansaho amesisitiza kuwa kiwanda hicho kitakuwa na mchango mkubwa si kwa Shirika la Mzinga na JWTZ pekee, bali pia kwa Mkoa wa Arusha na Taifa kwa ujumla.
Amebainisha kuwa kupitia uzalishaji wa kokoto, mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa malighafi muhimu kwa sekta ya ujenzi, kuchochea maendeleo ya miundombinu, kuunda fursa za ajira, kukuza biashara za usafirishaji na huduma nyingine zinazohusiana na uzalishaji, pamoja na kuongeza mapato ya Serikali.
Aidha, Waziri wa Ulinzi na JKT amezitaka taasisi na mashirika yaliyo chini ya sekta ya ulinzi kuimarisha ubunifu na kuweka mkazo katika uwekezaji mkubwa wa kimkakati wenye uwezo wa kuzalisha mapato endelevu.
Amesema kuwa taasisi hizo zinapaswa kutumia rasilimali na uwezo zilizopo kuanzisha miradi yenye tija ya kiuchumi, itakayochangia kujitegemea kifedha na kuimarisha mchango wa sekta ya ulinzi katika maendeleo ya Taifa.
Ameongeza kuwa taasisi za kijeshi zinapoendeshwa kwa weledi, nidhamu na kuzingatia misingi imara ya kibiashara, zina uwezo mkubwa wa kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.
