Riyadh
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Kifalme ya Saudi Arabia zimesaini makubaliano ya ushirikiano (MoU) katika sekta ya nishati ambapo ushirikiano huo utahusisha pia kampuni za mafuta, gesi na umeme katika nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yametiwa saini na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera na Mwanamfalme Abdulaziz bin Salman Al Saud, Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia pembezoni mwa Mkutano wa 25 wa WPC (25th WPC Congress) unaoendelea jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Dkt. Homera amesema suala hilo limewezekana baada ya wataalam wa pande zote mbili kufanya kazi kwa ufanisi kwa muongozo na maelekezo ya Wakuu wa nchi lengo likiwa ni kufungua ukurasa wa kushirikiana katika sekta ya nishati ambayo nchi ya Saudi Arabia imepiga hatua kubwa.
Ametaja maeneo ambayo Tanzania na Saudi Arabia wamekubaliana kushirikiana kuwa ni upatikanaji wa bidhaa za mafuta kupitia mikataba ya kibiashara, uendelezaji wa miundombinu ya bidhaa za mafuta ikiwemo ya usafirishaji na uhifadhi, tathmini ya fursa zitokanazo na mradi wa LNG, kubadilishana ujuzi na utaalam katika eneo la utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi na kutafiti fursa za uendelezaji wa viwanda vya bidhaa zitokanazo na mafuta na gesi (petrochemicals).
Maeneo mengine ya ushirikiano ni umeme na nishati jadidifu, kuchochea ufanisi katika matumizi ya nishati, kubadilishana teknolojia na suluhisho la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia, biashara ya kaboni, kutafiti fursa zinazohusiana na programu ya uendelevu wa nishati, matumizi ya akili mnemba katika sekta ya nishati na mapinduzi ya kidijitali pamoja na kujengeana uwezo na kubadilisha uzoefu katika sekta ya nishati kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwanamfalme Abdulaziz bin Salman Al Saud, Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia amesema “utiaji saini wa makubaliano haya ni zaidi ya kusaini karatasi, ni pambazuko la siku mpya inayoanza na tumaini jipya lenye kuweka maslahi ya watu wa Tanzania na Saudi Arabia katikati ya kila uamuzi kuhusu nishati, nchi zetu zimekuwa marafiki kwa miaka mingi na sasa tunayo fursa ya kubadili urafiki huo kuwa undugu kwa kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo kubadilisha utaalamu, ujuzi na kushirikiana katika miradi ya maendeleo inayohusu nishati.” Amesema
Hafla hiyo ya utiaji saini makubaliano hayo ilishuhudiwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mhandisi Zena Ahmed Said pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).