Uncategorized

BoT YAWEKA MIKAKATI YA KULINDA UTHABITI WA SEKTA YA FEDHA DHIDI YA MABADILIKO YA TABIANCHI

Written by Alex Sonna

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kuimarisha juhudi za kuingiza masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika usimamizi wa sekta ya fedha, kwa lengo la kulinda uthabiti wa mfumo wa fedha na kuongeza uwekezaji katika miradi inayojenga ustahimilivu wa uchumi.
Hatua hizo zimeelezwa katika Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaofanyika jijini Antalya, Uturuki, ambapo BoT kwa kushirikiana na Mtandao wa Benki Kuu na Mamlaka za Usimamizi wa Sekta ya Fedha kwa ajili ya Kuhamasisha Mfumo wa Fedha Rafiki kwa Mazingira (NGFS), iliandaa mijadala miwili tarehe 12 na 13 Novemba 2026.
Akifungua mjadala wa kwanza, Meneja wa Idara ya Uthabiti wa Sekta ya Fedha wa BoT, Bi. Edista Njau, alisema mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa vihatarishi vinavyoathiri uchumi na sekta ya fedha, hivyo kuna umuhimu wa taasisi za fedha kuimarisha uwezo wa kutathmini na kukabiliana na athari zake.
Alieleza kuwa BoT imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo kutoa miongozo ya usimamizi wa vihatarishi vya tabianchi na kuhimiza taasisi za fedha kufanya tathmini na majaribio ya uwezo wa kuhimili mishtuko inayotokana na mabadiliko hayo.
Akichangia mjadala huo, Mchambuzi na Mtaalamu wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Uendelevu BoT , Bw. Joseph Kenene, alisema BoT inaendelea kuanzisha Kanzidata ya Tabianchi itakayounganisha taarifa za kifedha na takwimu za mazingira ili kuboresha tathmini ya vihatarishi na maamuzi ya utoaji mikopo.
Katika mjadala wa pili uliohusu kupunguza pengo la ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Meneja Msaidizi wa Idara ya Uthabiti wa Sekta ya Fedha, Dkt. Method Simbachawene, alisisitiza umuhimu wa kurahisisha masharti ya upatikanaji wa fedha za tabianchi kutoka taasisi za kimataifa na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi.
Alibainisha kuwa mikopo yenye masharti nafuu, dhamana za mikopo na hati fungani za kijani ni miongoni mwa mifumo bunifu inayoweza kuongeza uwekezaji katika sekta muhimu kama kilimo, maji na miundombinu himilivu.
Kupitia ushiriki huo, BoT imepata fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kujenga uwezo wa watumishi kupitia programu za mafunzo, ikiwemo zinazotolewa na Benki Kuu ya Ujerumani.

About the author

Alex Sonna