Jumatatu, Novemba 23, 2026
HABARI MPYA
Kimataifa

RAIS SAMIA AZINDUA MPANGO ELEKEZI WA AFYA YA MAMA NA  MTOTO BARANI AFRIKA 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, akizungumza kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026) Jijini Addis Ababa nchini Ethiopia. Mkutano huo mkubwa wa kimataifa unawakutanisha viongozi wa Serikali, mawaziri wa afya, wataalamu wa afya, wanasayansi, watafiti na washiriki wa maendeleo kutoka Afrika na duniani.

….

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,amezindua Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika. 

Uzinduzi huo umefanyika leo, tarehe 23 Novemba, 2026, Addis Ababa, Ethiopia, katika Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026). 

Rais Dkt. Samia, ambaye pia ni Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, amezitaka nchi za Afrika kuharakisha hatua za kukomesha vifo vya uzazi na watoto  wachanga, vinavyoweza kuzuilika. 

“Kulinda akina mama, kuwalinda watoto na kuwekeza kwa vijana ni majukumu ya  msingi ya uongozi,” amesema Rais Dkt. Samia, akiongeza kuwa hatua hizo zinahitaji  ufadhili endelevu na uwajibikaji thabiti. 

Akiwasilisha muktadha wa bara la Afrika, amesema mwaka 2023, wanawake takriban  180,000 walifariki kutokana na sababu za uzazi, huku watoto wachanga milioni 1.18  wakipoteza maisha. 

Nchini Tanzania, amesema Rais Dkt. Samia, utafiti mpya unaonesha vifo vya uzazi  vimeshuka hadi takribani 75 kutoka vifo 104 vya awali, kwa kila vizazi hai 100,000. 

Amesema kutambuliwa kwa mafanikio ya Tanzania na Gates Foundation kumehamasisha  juhudi zaidi za kupunguza vifo hivyo nchini. Amebainisha kuwa uzinduzi wa matokeo ya  utafiti huo yatafanyika tarehe 26 Novemba, 2026 jijini Dar es Salaam. 

Mpango Elekezi unaweka malengo ya Sifuri Tatu kwa nchi wanachama wa Umoja wa  Afrika, ikiwemo kuhakikisha kila mjamzito anajifungulia katika kituo cha afya  akihudumiwa na mtaalamu. 

Malengo mengine ni kukomesha vifo vya uzazi na vya watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika, pamoja na kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo.

Ili kufanikisha utekelezaji wa mpango uliozinduliwa, Rais Dkt. Samia amezitaka nchi  wanachama kuteua waratibu wenye mamlaka na kuingiza malengo ya Mpango Elekezi katika utekelezaji wa mikakati yao ya kitaifa ya afya. 

Katika kuimarisha wataalamu wa sekta ya afya, Rais Dkt. Samia ametangaza ufadhili wa  awali wa nafasi 60 za mafunzo ya ubobezi kwa nchi za Afrika. 

Mafunzo hayo yatahusisha ukunga, usingizi na ganzi, uzazi na magonjwa ya wanawake,  pamoja na huduma kwa watoto wachanga, sambamba na mafunzo mafupi na ya vitendo  chini ya usimamizi wa wataalamu wa tiba wa ngazi ya kati, wauguzi na wakunga. 

Mkutano wa CPHIA 2026 umehudhuriwa, pamoja na washiriki wengine, na Wakuu wa  Nchi na Serikali wa Afrika, akiwemo Rais wa Burundi na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika,  Mheshimiwa Évariste Ndayishimiye; Rais wa Sierra Leone, Mheshimiwa Dkt. Julius Maada  Bio; na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mheshimiwa Dkt. Abiy Ahmed Ali. 

Wengine ni Makamu wa Rais wa Uganda, Mheshimiwa Jessica Alupo, na Waziri Mkuu wa  Rwanda, Mheshimiwa Dkt. Justin Nsengiyumva. 

Mkutano huo unaendelea jijini Addis Ababa, ukijadili hatua za kupunguza utegemezi wa  misaada ya kutoka nje, na kuongeza ufadhili wa ndani na uzalishaji wa dawa na chanjo barani Afrika. 

Halikadhalika, Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, na  Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) zitaendesha  mazungumzo ya ngazi ya juu tarehe 24 Novemba, 2026, jijini Addis Ababa, kuhusu  utekelezaji wa mpango uliozinduliwa. 

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amekutana na kuzungumza na Waziri Mkuu wa  Ethiopia, Mheshimiwa Dkt. Abiy Ahmed Ali, pamoja na Waziri wa Nchi, Wizara ya Mambo  ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mheshimiwa Sheikh Shakhboot bin Nahyan Al  Nahyan, pembezoni mwa mkutano wa CPHIA 2026, jijini Addis Ababa.  


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,
akisalimiana na Mhe. Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia baada ya kuwasili katika Kituo cha Mikutano cha African International Convention Centre (AICC), Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya kushiriki kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), tarehe 23 Novemba, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,akiwa pamoja na viongozi mbalimbali kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), Jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 23 Novemba, 2026.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,
akiwa kwenye mazungumzo na Mhe. Julius Maada Bio, Rais wa Sierra Leone baada ya kuwasili katika Kituo cha Mikutano cha African International Convention Centre (AICC), Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya kushiriki kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), tarehe 23 Novemba, 2026.

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (CDC) Dkt. Jean Kaseya baada ya kuwasili katika Kituo cha Mikutano cha African International Convention Centre (AICC), Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya kushiriki kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), tarehe 23 Novemba, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Mhe. Evariste Ndayishimiye, Rais wa Jamhuri ya Burundi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), baada ya kuwasili katika Kituo cha Mikutano cha African International Convention Centre (AICC), Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya kushiriki kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), tarehe 23 Novemba, 2026.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassanakiwa na Mhe. Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, kwenye picha na viongozi mbalimbali wanaoshiriki kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), Addis Ababa, Ethiopia, tarehe 23 Novemba, 2026.