Featured Kimataifa

RAIS SAMIA ATETA NA RAIS WA MISRI NCHINI MISRI

Written by mzalendoeditor

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah El-Sisi mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya Rais El- Sisi katika Mji wa Sharm El Sheikh, nchini Misri

……………………….

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amekutana na Rais wa Jamhuri ya Misri, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi, leo kwenye mji wa Sharm El Sheikh.

Katika mkutano huo, viongozi hao wamezungumzia masuala mbalimbali yanayohusu uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili hasa kuwepo kwa mikakati mahsusi ya kuongeza kasi ya biashara na uwekezaji.  

Marais hao wamezungumzia ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere unaojengwa na wakandarasi kutoka Misri na kuonyesha kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo uliofikia 77% mpaka sasa. 

Vilevile, Rais Samia amemueleza Rais El-Sisi kwamba Tanzania ina mpango wa kuziba njia ya kuchepusha mto na kuanza kujaza maji kwenye bwawa hilo. Rais El-Sisi ameahidi kutuma ujumbe mzito katika tukio hilo muhimu. 

Viongozi hao wawili wamesisitiza umuhimu wa kuutekeleza mradi huo kwa ubora na viwango vya uhakika hata kama utachelewa nje ya muda uliotarajiwa hapo awali.

Pia Marais hao wamesisitiza kuwa timu ya wataalamu wa pande zote mbili wafanye kazi kwa karibu ili kutatua changamoto ndogondogo zinazojitokeza kwenye mradi huo.

Katika mkutano huo, Rais Samia aliongozana na Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Balozi wa Tanzania nchini Misri, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah El-Sisi mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya Rais El- Sisi katika Mji wa Sharm El Sheikh, nchini Misri

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Ujumbe wake akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah El-Sisi kwenye Ofisi ya Rais El-Sisi katika Mji wa Sharm El Sheikh, nchini Misri

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah El-Sisi baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika kwenye Ofisi ya Rais El-Sisi katika Mji wa Sharm El Sheikh, nchini Misri 

About the author

mzalendoeditor