Featured Kimataifa

ALIYEPIGILIWA MISUMARI KWENYE MTI TUHUMA ZA WIZI WA REDIO AFUNGUKA

Written by mzalendoeditor
Kijana akiwa amepigiliwa misumari kwenye mti 
Kijana akiwa hospitali
**
Kijana wa miaka 19 kutoka kijiji kimoja kaunti ya Vihiga amelazwa katika hospitali ya Itando Mission baada ya jeraha la misumari.
Collins Sambaya alisurubishwa kwenye mti kwa kupigwa misumari katika mkono wake baada ya kushukiwa kuiba kifaa cha muziki. 
Kisa hicho cha Februari 18,2022 kimewaacha wengi kinywa wazi ni vipi washukiwa walitekeleza unyama huo baada ya kumshuku kijana huyo aliiba kifaa hicho cha KSh 6000 sawa na shilingi 126,000 ya Tanzania
Sambaya aliambia wanahabari kuwa aliteswa na washukiwa ambao ni watu anawajua wakidai alipora kifaa hicho. 
Walichukua nyundo na kupiga mkono wake msumari kwenye mti kama adhabu ya kuwapora na kisha wakaingia mitini. 
Picha za mvulana huyo mkono wake ukiwa kwenye mti huku msumari ukiushikisha zilipepea kwenye mitandao.
“Niliwaomba kunisamehe lakini hawakuskia chochote,” kijana huyo aliambia runinga ya Citizen akiwa katika hospitali anapouguza majeraha.
Hapo awali babu yake Sambaya alisema washukiwa walifika nyumbani na kumhadaa kijana huyo kuwafuata mpaka boma ambapo wizi huo ulifanyika.
 “Kisa hicho kilifanyika saa nane mchana lakini tulikuwa tunapata habari saa kumi na moja jioni. Washukiwa walikuja nyumbani na kumhadaa mjukuu wangu awafuate,” alisema babu yake Sambaya.
 Mzee huyo alisimulia kuwa kijana huyo siku kadhaa kabla ya kusulubishwa alikuwa amekamatwa na polisi kwa madai ya kuwa mshukiwa wa wizi huo. Hata hivyo, polisi wlaimwachilia na ndipo washukiwa wakamkujia na kufanyia kitendo hicho.
Polisi wanaendelea kusaka waliotekeleza kisa hicho ikidaiwa waliingia mitini baada ya kujua kitumbua chao kimeingia mchanga.
 
 “Wanakijiji ambao hawakuamini kile kilikuwa kimefanyika kwa mmoja wao waliangalia kwa umbali huku polisi wakimuokoa kijana huyo. Washukiwa wanasakwa,” polisi walisema.

About the author

mzalendoeditor