📍 Paris, Ufaransa
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa rai
kwa Wafanyabiashara wa Ufaransa kuwekeza kwenye uongezaji thamani madini mkakati nchini Tanzania kwa kujenga viwanda vya kuchenjua, kusafisha na kuyeyusha madini.
Waziri Mkuu Nchemba ameyasema hayo leo tarehe 6.07.2026 Jijini Paris,Ufaransa wakati wa mkutano wa kibiashara baina ya sekta binafsi ya Ufaransa na Tanzania wenye lengo la kubainisha fursa za kiuchumi na ushirikiano baina ya nchi mbili za Tanzania na Ufaransa.
“Tanzania imebarikiwa kuwa na madini mengi yakiwemo madini ya kimkakati ambayo leo dunia inayahitaji sana,ni wakati muafaka kufikiria ujenzi
Wa viwanda vya kuongeza thamani madini eneo ambalo una uhakika wa malighafi ya kutosha.
Nawakaribisha kuja kuwekeza Tanzania, nchi yenye sera zinazotabirika,vivutio vizuri vya uwekezaji na mazingira rafiki ya kufanya biashara ambayo yamesimamiwa vyema kwa maelekezo ya Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan,” amesema Mhe. Mwigulu.
Naye ,Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema uongezaji thamani madini ni takwa muhimu la Sera ya Madini na kwamba serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya kiuwekezaji ili kuvutia uwekezaji mkubwa kwenye kusafisha,kuchakata na kuyeyusha madini ndani ya nchi ya Tanzania
Naye, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Bi. Angelina Ngalula amesisitiza juu ya umuhimu wa ushirikiano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Ufaransa katika kusaidia kuongeza ujuzi,matumizi sahihi ya teknolojia na kukuza mitaji ili kufanya biashara kwa urahisi.
