Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuanzisha mfumo wa ulinganishaji wa ada na tozo za mikopo unaolenga kuongeza uwazi na kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi kabla ya kukopa.
Pongezi hizo zimetolewa leo, Ijumaa, Oktoba 23, 2026, wakati BoT ikiwasilisha mada mbili kwa wajumbe wa kamati hiyo, zinazohusu utendaji wa mfumo wa ulinganishaji wa ada na tozo za mikopo pamoja na mfumo wa utekelezaji wa sera ya fedha unaotumia riba.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji huo, Mwenyekiti wa kamati hiyo na Mbunge wa Maswa Magharibi, Mhe. Mashimba Ndaki, amesema mfumo huo utawasaidia wananchi kulinganisha gharama za mikopo kutoka taasisi mbalimbali za fedha na kufanya maamuzi yanayozingatia uwezo wao wa kifedha.
“Mfumo huu utasaidia kuwafanya wananchi wajue viwango vya ada na tozo katika mikopo, lakini pia uwazi huu utasababisha wafanye machaguo sahihi. Tunawapongeza kwa hilo,” amesema Ndaki.
Aidha, kamati hiyo imeitaka BoT kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma ili wananchi wengi zaidi wafahamu matumizi ya mfumo huo na namna unavyoweza kuwasaidia kupata taarifa za gharama za mikopo kabla ya kufanya maamuzi ya kukopa.
Ndaki amesema ni muhimu mfumo huo kusambazwa kupitia majukwaa mbalimbali ya kidijitali, pamoja na huduma za simu zinazotumia msimbo wa USSD, ili kurahisisha upatikanaji wake kwa wananchi wengi zaidi.
Mfumo wa ulinganishaji wa ada na tozo za mikopo ni miongoni mwa jitihada zinazolenga kuwawezesha watumiaji wa huduma za fedha kupata taarifa zinazowasaidia kuelewa gharama za mikopo kabla ya kuingia katika mikataba na taasisi za fedha.




