Kankonko, Kigoma
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Kakonko imekabidhi Mikataba (23) kwa vikundi vya kijamii kwa lengo la kufanya matengenezo ya kawaida ya barabara yenye thamani ya shilingi milioni 211 kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Akikabidhi mikataba hiyo Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Zuma Ally amevitaka vikundi hivyo kufanya kazi kwa bidii kwani ni vikundi vya mfano na hivyo wananchi wengine waweze kunufaika na shughuli hizo za CBRM.
Amesema awali fedha hizo zilikuwa zikilipwa kwa wakandarasi wakubwa kutoka nje ya wilaya hivyo watumie fursa hiyo kufanya kazi na kujiimarisha kiuchumi.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kakonko Bw. Ndaki Mhuli amevitaka vikundi hivyo kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maelekezo yote watakayopewa na wataalam wakati wanatekeleza kazi hizo.
“Wana vikundi mnatakiwa kuhakikisha barabara zinakuwa safi na zinapitika wakati wote, pia mnatakiwa kuomba kazi mbalimbali zinazotangazwa na halmashauri ili kuboresha maisha na hili ndiyo lengo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Awali, Afisa Maendeleo wa Halmashauri ya Kakonko Bi. Eusebia Barantonda, amesema vikundi hivyo vimesajiliwa katika mfumo wa NeST kwa ajili ya kupata kazi mbalimbali ikiwemo hizo za matengenezo ya kawaida ya barabara kupitia shughuli za CBRM ambayo itakuwa fursa nzuri kwa vikundi kuongeza kipato na kupata ajira.
Ametaja vikundi hivyo vipo vikundi vya Vijana 15, Wanawake 06, Wazee kikundi 01 na Walemavu kikundi 01.
Naye, Kaimu Meneja wa TARURA mkoa wa Kigoma Mhandisi John Ambrose ambaye ni Meneja wa wilaya ya Kakonko amesema katika wilaya hiyo jumla ya Kilomita 140.3 zitatekelezwa kupitia shughuli za CBRM kwa kutumia vikundi hivyo 23 na kuongeza kwamba wanategemea matokeo mazuri kwa vikundi vilivyopata fursa hiyo.
Pia, Mratibu wa Shughuli za CBRM mkoa wa Kigoma Mhandisi Juma Mdoe amesema lengo la CBRM ni kuondoa umaskini katika kaya, kuongeza umiliki wa barabara ikiwa ni pamoja na kulinda mazingira na miundombinu ya barabara ili kuhakikisha zinapitika kwa nyakati zote.
