ZAIDI ya washiriki 200 wanatarajiwa kushiriki Jukwaa la Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar na Mkutano Kivuli wa Mabadiliko ya Tabianchi (ZANCCC), linaloanza leo kujadili masuala ya mazingira, uchumi wa buluu na maendeleo endelevu.
Jukwaa hilo lililoandaliwa na Jumuiko la Taasisi za Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar (ZACCA), linatarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Anna Athanas Paul, katika Chuo cha Utalii Maruhubi, Unguja, na kuendelea hadi Oktoba 26 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa ZACCA, Mahfoud Haji, alisema jukwaa hilo litawakutanisha wadau wa serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na wanaharakati wa mazingira kujadili changamoto za sekta hiyo na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana nazo.
Alisema mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa mikakati ya uhifadhi wa mazingira na kuhamasisha matumizi ya fursa zinazotokana na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Alieleza kuwa washiriki kutoka Tanzania na nchi nyingine, zikiwemo Ujerumani, Ethiopia na Kenya, watashiriki majadiliano yatakayojikita katika masuala ya kimkakati yanayohusu mazingira, uchumi wa buluu na maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa Haji, katika siku tatu za mkutano huo kutakuwa na maonesho ya shughuli za taasisi zinazojihusisha na mazingira pamoja na vipindi 12 vya majadiliano vitakavyohusisha wataalamu wa serikali, wizara na wadau wa ndani na nje ya nchi.
Alisema mada zitakazojadiliwa ni pamoja na kuendeleza uchumi wa buluu kwa njia endelevu, kutumia taka kama chanzo cha fursa za kiuchumi na kuimarisha matumizi ya nishati safi.
Alisisitiza kuwa uchumi wa buluu ni muhimu kwa Zanzibar kutokana na fursa zilizopo katika rasilimali za bahari, hivyo ni lazima shughuli za kiuchumi ziendelezwe bila kuharibu mazingira.
Kuhusu taka, alisema majadiliano yataangazia namna ya kuzibadili kuwa bidhaa zenye thamani, ikiwemo mbolea, ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza fursa za ajira na kipato.
Aliongeza kuwa jukwaa hilo litakuwa na vipengele vitatu vikuu ambavyo ni maonesho ya shughuli za wadau wa mazingira, majadiliano ya kitaalamu na utoaji wa tuzo kwa vinara wa mazingira Zanzibar.
Alisema kilele cha shughuli hizo kitakuwa Oktoba 26, kwa kufanyika kwa usiku wa tuzo za vinara wa mazingira katika ukumbi wa Palm Hall, Mombasa, Wilaya ya Magharibi ‘B’, Unguja, kwa lengo la kutambua mchango wa wadau katika uhifadhi wa mazingira na kuhamasisha jamii kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mjini, Mohammed Ibrahim Hassanali ‘Razalee’, aliipongeza ZACCA na wadau wengine kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kudhibiti taka na kuboresha usafi wa miji.
Alisema jukwaa hilo litatoa fursa kwa taasisi za serikali, ikiwemo manispaa, kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kusimamia taka na kuzitumia kama fursa za kiuchumi.
Razalee alisema ubunifu wa kuzalisha mbolea na bidhaa nyingine kutokana na taka unaweza kuongeza shughuli za uzalishaji na kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato.
Aliongeza kuwa Manispaa ya Mjini ina mikakati ya kuimarisha usafi wa mazingira sambamba na uwekezaji unaofanywa na Serikali Kuu chini ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Alitaja baadhi ya miakati hiyo kuwa ni pamoja na kushiriiana na vikosi vya Idara maalum za SMZ na kutafufa muwekezaji mwenye uwezo wa kusafisha, kusanya na kusarifu taka ili kupunguza kadhia ya uchafu atia maeneo ya manispaa hiyo.