Featured Kitaifa

MAWAZIRI WAKUTANA KUJADILI UCHUMI WA BULUU

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamadi Yusuf Masauni (aliyeketi mbele) akiongoza kikao cha Mawaziri cha kuwasilisha mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli za Uchumi wa Buluu nchini kwa mwaka 2024/25 na 2025/26 kilichofanyika Dodoma

……

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.Mhandisi Hamad Yusuf Masauni amesemea Uchumi wa Buluu ni dhana inayochagiza ukuaji wa uchumi kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za maji kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira na ushirikishwaji wa jamii. 

Amesema hayo wakati wa kikao cha Mawaziri cha kuwasilisha mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli za Uchumi wa Buluu nchini kwa mwaka 2024/25 na 2025/26 kilichofanyika Dodoma Februari 13, 20205. 

“Shughuli za Uchumi wa Buluu hapa nchini zinatekelezwa kwa sera, sheria, miongozo, mikakati na mipango ya kisekta ikiwemo, Uvuvi, Nishati, Uchukuzi, Maliasili na Utalii, Maji, Umwagiliaji, Viwanda na Biashara, Uhifadhi wa Mazingira, Madini, na Uwekezaji.

“Pamoja na uwepo wa sera na sheria hizo, kumekuwepo na changamoto mtambuka zinazochangia Taifa kutonufaika ipasavyo na rasilimali za Uchumi wa Buluu zikiwemo kukosekana kwa mfumo jumuishi wa kitaasisi wa uratibu wa shughuli za Uchumi wa Buluu, Kukosekana kwa Mpango wa Matumizi wa Maeneo ya Maji, Uwekezaji usio wa kimkakati na fungamanishi katika matumizi ya rasilimali za Uchumi wa Buluu na Uhaba wa utafiti na ujuzi katika matumizi ya rasilimali za Uchumi wa Buluu. 

Amesema kwa kuzingatia changamoto hizo na ili kufanikisha azma ya Serikali katika kutumia rasilimali za Uchumi wa Buluu ili kukuza uchumi wa Taifa kwa maendeleo endelevu, Serikali iliaandaa na kupitisha Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya Mwaka 2024 na Mkakati wake wa utekelezaji wa mwaka (2024-2034) iliyozinduliwa Juni 5, 2024.  

Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya Mwaka 2024 imezingatia maeneo muhimu ambayo ni Uratibu wa Shughuli za Uchumi wa Buluu ili kuwa na mfumo jumuishi wa uratibu miongoni mwa wadau wanaosimamia na kutekeleza shughuli za Uchumi wa Buluu nchini, Matumizi ya Maeneo ya Maji ili kuwezesha nchi kunufaika ipasavyo na fursa za Uchumi wa Buluu kwa kuzingatia mahitaji ya shughuli za kiuchumi, kijamii na uhifadhi wa mifumo ikolojia na mazingira na Usimamizi katika eneo la Ukanda Maalumu wa Uchumi wa Bahari na Bahari Kuu ili kuimarisha uratibu wa rasilimali zote za Uchumi wa Buluu katika eneo la Ukanda Maalumu wa Uchumi wa Bahari na Bahari Kuu. 

Waziri Masauni ameongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kama Msimamizi Mkuu wa Masuala ya Uchumi wa Buluu nchini, imepewa jukumu la kuratibu utekelezaji wa shughuli za Uchumi wa Buluu Tanzania Bara kwa kuratibu, kufuatilia na kufanya tathmini ya utekelezaji shughuli zote za uchumi wa buluu ikiwemo shughuli zinazotekelezwa na sekta zenye Mnasaba na Masuala ya Uchumi wa Buluu. 

”Kwa mantiki hiyo, OMR kwa kushirikiana na Sekta zenye mnasaba na masuala ya uchumi wa buluu iliandaa Mpangokazi wa Utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Buluu kwa mwaka 2024/25 na 2025/26. Aidha, kwa mwaka 2024/25 shughuli zilizoainishwa zinatarajiwa kukamilika kutekelezwa katika hii nusu ya pili ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25.”

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema lengo ni kunufaika na rasilimali zilizopo na nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha mwelekeo wa nini kifanyike katika eneo hili.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa mwaka 2023, sekta ya uvuvi imeendelea kukua na kutoa mchango mkubwa katika ajira na usalama wa chakula, uzalishaji wa mazao ya uvuvi unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 473,592 hadi tani 639,092, sawa na ongezeko la asilimia 34.9 kwa mwaka 2024.   

 

Kwa Tanzania, Uchumi wa Buluu unajumuisha shughuli za kiuchumi zilizoendelevu zinazohusiana na bahari, maziwa, mito, mabwawa, Maeneo Oevu na maji chini ya ardhi kwa manufaa ya jamii bila kuathiri mazingira. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamadi Yusuf Masauni akizungumza wakati wa kikao cha Mawaziri cha kuwasilisha mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli za Uchumi wa Buluu nchini kwa mwaka 2024/25 na 2025/26 kilichofanyika Dodoma

    

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamadi Yusuf Masauni (aliyeketi mbele) akiongoza kikao cha Mawaziri cha kuwasilisha mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli za Uchumi wa Buluu nchini kwa mwaka 2024/25 na 2025/26 kilichofanyika Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamadi Yusuf Masauni (katikati) akimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja (aliyesimama) wakati wa kikao cha Mawaziri cha kuwasilisha mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli za Uchumi wa Buluu nchini kwa mwaka 2024/25 na 2025/26 kilichofanyika Dodoma Februari 13, 2025. Wa kwanza kushoto ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari

About the author

mzalendoeditor