Featured Kitaifa

MAPINDUZI YA HAKI: NJIA MBADALA ZA UTATUZI WA MIGOGORO ZAVUNJA REKODI TANZANIA

Written by Alex Sonna

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo  na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2026/27, leo, tarehe 24 Aprili 2026, Bunge jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

Katika kipindi ambacho mifumo ya mahakama imekuwa ikikabiliwa na ongezeko la mashauri, Tanzania imeanza kushuhudia mageuzi makubwa kupitia matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro (ADR), hatua inayochukuliwa kama mkombozi wa haki ya haraka na nafuu kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 24,2026 bungeni Dodoma.

Amesema kuwa kati ya Julai 2025 hadi Machi 2026, juhudi za makusudi zimewekwa katika kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi ili kuhakikisha huduma za usuluhishi, upatanishi na majadiliano zinakuwa chaguo la kwanza kwa wananchi.

Katika kipindi hicho, maombi 332 ya wataalam wa utatuzi wa migogoro yalipokelewa, ambapo 205 yaliidhinishwa ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Hadi kufikia Machi 2026, wataalam 881 walikuwa wamesajiliwa rasmi, wakionyesha kukua kwa kasi kwa sekta hii muhimu.

Wataalam hao wamejengewa uwezo kupitia mafunzo maalum, wakiwemo wasuluhishi 362, wapatanishi 286, waendesha maridhiano 101 na waendesha majadiliano 132. Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vya kitaaluma na matarajio ya jamii.

Mbali na hilo, jitihada za kuelimisha umma zimeendelea kushika kasi. Kupitia Maonesho ya Sabasaba, wananchi 162 walipata elimu juu ya umuhimu wa kutumia njia hizi, huku changamoto ya uelewa mdogo wa jamii ikiendelea kushughulikiwa kwa mikakati mbalimbali ya kitaifa.

Katika hatua ya kuimarisha zaidi mfumo huu, Wizara imeanzisha Kitengo maalum cha Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala, kinachotarajiwa kuratibu huduma hizi kwa ufanisi zaidi na kupunguza utegemezi wa mahakama katika utatuzi wa migogoro ya kiraia.

Takwimu zinaonesha mafanikio makubwa ya kifedha. Kupitia majadiliano yaliyosimamiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, migogoro ya madai 143 yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 2.8 ilishughulikiwa. Baada ya majadiliano, madai yalipunguzwa hadi trilioni 2.18, hivyo kuiwezesha Serikali kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 646 fedha ambazo zingeweza kupotea kama kesi zingesikilizwa mahakamani.

Katika ngazi ya jamii, hatua zimechukuliwa kusogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi. Jumla ya wajumbe 344 wa Bodi za Usuluhishi wa Ndoa wameteuliwa katika halmashauri mbalimbali, wakisaidia kutatua migogoro ya kifamilia kwa haraka na kwa kuzingatia maridhiano badala ya migogoro mirefu ya kisheria.

Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi nacho kimeonesha mafanikio makubwa, ambapo kati ya mashauri 275 yaliyokuwepo hadi Machi 2026, mashauri 242 yamesuluhishwa kwa mafanikio. Hii ni ishara tosha kuwa njia mbadala zinaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa mlundikano wa kesi mahakamani.

Katika kuendeleza mafanikio haya, Mahakama ilizindua Wiki ya Usuluhishi Aprili 2026 jijini Dar es Salaam, ikifuatiwa na utoaji wa elimu na huduma bure nchi nzima. Wananchi walipata fursa ya kuelewa na kunufaika na mfumo huu ambao unahimiza maelewano badala ya migogoro.

About the author

Alex Sonna