Na Edward Winchislaus-DODOMA
WAKATI Serikali ikiendelea kuhimiza ongezeko la uzalishaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imesema mafanikio ya sekta hizo yanategemea pia uwepo wa nguvu kazi yenye afya, hivyo imeendelea kusisitiza umuhimu wa kinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ili kulinda maendeleo ya uchumi wa taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 7, 2026, katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt. Adam Mrisho, amesema afya bora ndiyo nguzo ya maendeleo ya taifa, akiwataka hasa vijana kuendelea kujikinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ili waendelee kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na ujenzi wa uchumi.
Amesema maambukizi ya Virusi vya UKIMWI yameendelea kuathiri kipato cha familia na maendeleo ya taifa kwa ujumla jambo linaloifanya Serikali kuendelea kuwekeza katika kinga, elimu na matibabu kwa lengo la kulinda ustawi wa wananchi.
“Kwa miaka mingi Tanzania imenufaika na ushirikiano wa wadau wa maendeleo, wakiwemo Global Fund na Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR), ambao umechangia upatikanaji wa huduma za upimaji, elimu, dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARVs) pamoja na huduma nyingine muhimu bila malipo.”amesema Dkt. Mrisho
Hata hivyo,amesema kutokana na mabadiliko ya mazingira ya ufadhili duniani na kupungua kwa misaada kutoka kwa baadhi ya wahisani, Serikali ilianzisha AIDS Trust Fund mwaka 2015 ili kuhakikisha mapambano dhidi ya UKIMWI yanakuwa endelevu kupitia rasilimali za ndani.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuuchangia mfuko huo kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo ili kuhakikisha huduma za kinga, upimaji, elimu na dawa za ARVs zinaendelea kupatikana kwa wananchi bila kukwama.
Aidha, TACAIDS imeendelea kuratibu mwitikio wa taifa dhidi ya UKIMWI kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali huku ikiweka mikakati ya kuongeza rasilimali za ndani na kupunguza utegemezi wa wafadhili wa nje.
Dkt. Mrisho amesema makundi yanayojishughulisha na kilimo, mifugo na uvuvi yanapaswa kuendelea kufikiwa na huduma za kinga na elimu ya UKIMWI kwa kuwa ndiyo msingi wa nguvu kazi inayochochea uzalishaji na ukuaji wa uchumi.
Amesema ushiriki wa TACAIDS katika Maonesho ya Nanenane unalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa elimu kuhusu kinga dhidi ya Virusi vya UKIMWI, upimaji wa hiari na matumizi sahihi ya huduma zinazotolewa na Serikali, ili kujenga taifa lenye afya, nguvu kazi imara na uchumi endelevu.
