Nzega, Tabora
Serikali imepongezwa kwa kuendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kupitia ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya katika kila kata na kijiji, hatua inayotekelezwa kupitia Mpango wa MAM na ambayo imeongeza fursa kwa Watanzania kupata huduma bora za afya.
Pongezi hizo zimetolewa leo Agosti 7, 2026 na Mgeni Rasmi, Peter Mashili, wakati wa Mahafali ya Nne ya wahitimu wa ngazi ya Stashahada (Diploma) katika Chuo cha Uuguzi Nzega, ambapo amesema mafanikio ya mpango huo yanahitaji kuungwa mkono na upatikanaji wa wataalamu wenye weledi na maadili ya kazi.
Mashili pia amempongeza Rais wa Awamu ya sita Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia na kuwezesha Chuo cha Uuguzi Nzega kupata ithibati kamili (Full Accreditation) mwaka 2022, hatua iliyoleta ongezeko la hadhi ya chuo na kukiwezesha kuanza kutoa mafunzo ya ngazi ya Stashahada (Diploma). Amesema uamuzi huo umeongeza uwezo wa taifa kuzalisha wataalamu wa afya wenye sifa na umahiri wa kuhudumia wananchi katika vituo vya afya, zahanati na hospitali zinazozidi kujengwa nchini.
Katika kuunga mkono jitihada za kuboresha mazingira ya kujifunzia na utoaji wa mafunzo ya afya, Mgeni Rasmi Peter Mashili ametangaza kuchangia zaidi ya Shilingi milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa kichomea taka (incinerator) katika Chuo cha Uuguzi Nzega, pamoja na Shilingi milioni 5.5 kwa ajili ya ununuzi wa jenereta.
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya chuo hicho, Mashili amewapongeza wahitimu na uongozi wa chuo kwa kuendelea kudumisha viwango vya juu vya taaluma. Amesema kwa sasa chuo kina wanafunzi 143, ambapo 93 ni wasichana na 50 ni wavulana, hali inayoonyesha ushiriki mkubwa wa wanawake katika sekta ya elimu na taaluma ya uuguzi na ukunga.
Katika hatua nyingine, Mashili amekipongeza chuo hicho kwa mafanikio makubwa ikiwemo kwa kuendelea kutoa mafunzo ya Uuguzi na Ukunga, kupata hati miliki ya eneo la chuo lenye ukubwa wa ekari 7.68, kukarabati mabweni ya wasichana na wavulana pamoja na kuimarisha ushirikiano na Halmashauri ya Mji Nzega, Halmashauri ya Wilaya Nzega, Hospitali ya Mji Nzega na vituo vya afya vinavyozunguka chuo.
Naye Mkuu wa Chuo cha Uuguzi na Ukunga Nzega Bw Josephat K. Kaja amesema kuwa Mpango wa serikali wa kusogeza huduma za afya kwa wananchi kwa kujenga vituo vya kutolea huduma za afya katika kila kata, na kijiji ujulikanao kwa jina MAM, (Maendeleo ya afya Msingi) ndio ulio fanya serikali kuweka mikakati ya kufungua vyuo vilivyo fungwa kwa lengo la kutoa Mafunzo ya Wataalamu wa afya wa kwenda kutoa huduma za afya katika vituo vya kwenye kata na vijiji.
Kwa upande wa wanafunzi wahitimu wa mwaka wa tatu walimuomba mgeni rasmi kusaidia upatikanaji wa chanzo mbadala cha umeme kama Solar au Jenereta, pamoja na kujengewa kichomea taka (incinerator) ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na huduma za afya chuoni.
