Uncategorized

TANZANIA NA UJERUMANI ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA MAENDELEO KWA WANANCHI NA UCHUMI

Written by Alex Sonna

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pande Mbili kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida (kushoto), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango – Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi(katikati) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya (kulia), wakifuatilia mawasilisho mbalimbali yaliyokuwa yakiwasilishwa katika Mkutano wa Pande Mbili kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida (kushoto), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango – Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi (wa pili kushoto), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya (wa pili kulia) na Mkuu wa Kitengo cha Afrika Mashariki na Kati, Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani, Bw. Joachim Schmitt (kushoto), akifuatilia wasilisho la Tume ya Mipango Zanzibar katika Mkutano wa Pande Mbili kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, jijini Dodoma.

Mkuu wa Kitengo cha Afrika Mashariki na Kati, Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani, Bw. Joachim Schmitt akizungumza wakati wa Mkutano wa Pande Mbili kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida (kushoto), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango – Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi (wa pili kushoto), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya (wa pili kulia) na Mkuu wa Kitengo cha Afrika Mashariki na Kati, Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani, Bw. Joachim Schmitt (kushoto), wakisikiliza maelezo ya awali kutoka kwa Kamshna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Melckzedeck Mbise wakati wa Mkutano wa Pande Mbili kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, jijini Dodoma.

Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Pande Mbili kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, wakifuatilia mada mbalimbali katika mkutano huo, jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Aboud Hassan Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya na Mkuu wa Kitengo cha Afrika Mashariki na Kati, Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani, Bw. Joachim Schmitt wakiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa Mkutano wa Pande Mbili kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF Dodoma)

Na Farida Ramadhani na Asia Singano, WF- Dodoma

Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani zimeanza mazungumzo ya pande mbili kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa maendeleo, hususan katika miradi yenye matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi na Uchumi wa Taifa.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Fedha Mtumba, jijini Dodoma, yalijikita katika maeneo mbalimbali ya kimkakati, yakiwemo maji na usafi wa mazingira, afya, nishati, matumizi endelevu ya rasilimali za asili na uhifadhi wa mazingira, upatikanaji wa haki, usimamizi bora wa fedha za umma pamoja na usawa wa kijinsia.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa Pande Mbili, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, alisema mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Ujerumani, ambao una historia ya zaidi ya miongo sita.

Alisema ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani ulianza tangu miaka ya 1960, ambapo waasisi wa mataifa hayo waliweka misingi ya uhusiano na ushirikiano ambao umeendelea hadi sasa na mwaka 1975 Tanzania na Ujerumani zilisaini Mkataba wa Mfumo wa Ushirikiano (Framework Agreement) ulioweka misingi ya namna ushirikiano kati ya pande hizo mbili utakavyoendelezwa.

“Ujerumani imekuwa mshirika muhimu wa maendeleo kwa Tanzania katika sekta mbalimbali, zikiwemo maji, mawasiliano, utalii, maendeleo ya watu na ustawi wa jamii” Alisema Bw. Mwandumbya

Alisema kuwa majadiliano hayo yatawezesha wataalamu kutoka pande zote mbili kutathmini na kuweka vipaumbele vya miradi na maeneo ya ushirikiano yatakayotekelezwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Aliongeza kuwa baada ya timu za wataalamu kukamilisha majadiliano na kufikia makubaliano, Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ujerumani zinatarajiwa kuchukua hatua zinazofuata za kurasimisha makubaliano hayo, ikiwemo kusaini mkataba wa ushirikiano wa maendeleo na pia kuendekeza mazungunzo hayo mwezi Novemba 2026.

Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, alisema Tanzania iko tayari kuimarisha na kuhuisha ushirikiano wake wa muda mrefu na Ujerumani ili kuendana na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

Alisema Dira 2050 inalenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kipato cha kati cha juu, mseto, himilivu na jumuishi, huku ikihakikisha wananchi wanapata maisha bora na ustawi wa hali ya juu.

“Tanzania imejiwekea lengo la kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050 na kuongeza pato la Taifa kwa mtu mmoja hadi takribani dola 7,000, kutoka uchumi wa sasa unaokadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 90”, alisema Dkt. Kida.

Aliongeza kuwa pamoja na hayo, nchi inalenga kupunguza kwa kiasi kikubwa umaskini, kuondokana na umaskini uliokithiri na kukabiliana na umaskini wa chakula, sambamba na matumizi endelevu ya rasilimali na ulinzi wa mazingira na kwamba ushirikiano wa nchi hizo mbili utachangia kufikia malengo hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Afrika Mashariki na Kati, Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani, Bw. Joachim Schmitt, alisema Serikali ya Ujerumani itaendelea kushirikiana na Tanzania huku akibainisha mkakati mpya wa ushirikiano ambao utaelekezwa katika maeneo yenye uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kupunguza umaskini na ukosefu wa usawa, huku ikisisitiza umuhimu wa kulinda utawala wa sheria, nafasi ya asasi za kiraia, amani na usalama.

Alisema Ujerumani inataka ushirikiano huo uwe wa kimkakati zaidi na uendane na vipaumbele vya maendeleo ya Tanzania, badala ya kutegemea miradi midogo isiyounganishwa katika mwelekeo mpana wa maendeleo.

Bw. Schmitt, alisema Ujerumani imeweka msisitizo maalumu katika ushirikiano wa kiuchumi, maendeleo ya sekta binafsi na uwekezaji, ikilenga kuwashirikisha zaidi kampuni za Ujerumani na Tanzania katika miradi ya maendeleo.

Mkutano wa Mazungumzo hayo ya siku mbili, yamewakutanisha wawakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiongozwa na taasisi na wizara mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Katiba na Sheria, pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Na kwa upande wa Ujerumani umewakilishwa na Serikali ya Shirikisho la Ujerumani pamoja na taasisi zake za ushirikiano wa maendeleo, zikiwemo KfW na GIZ.

About the author

Alex Sonna