Wastani wa watoto 600,000 duniani, wanakadiriwa kudumaa akili kila mwaka kutokana na kuathiriwa na madini ya risasi yanayopatikana kwenye rangi.
Ripoti zinaonesha kuwa asilimia 90 ya watoto walioathiriwa kwa viwango vikubwa na madini ya risasi wanaishi kwenye nchi zenye uchumi wa kati na uchumi mdogo.
Kutokana na Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati, wadau wakuu wa usimamizi wa mazingira, afya na viwango nchini wamekutana Juni 30, jijini Dar es Salaam, kujadili na kupanga mbinu na mikakati ya kuharakisha kuondoa matumizi ya rangi zenye madini ya risasi (lead paint) nchini.
Hatua hiyo inalenga kulinda afya za wananchi na mazingira, ambapo Asasi isiyo ya Kiserikali ya AGENDA iliona haja ya kuendelea kushirikiana na wataalamu kutoka ndani ya taasisi za serikali katika kufanikisha mapambano hayo.
Wataalamu walioshiriki kwenye kikao kazi hicho ni Mhandisi Hassan Maalim, Mhandisi Geofrey Mtepa na Kulthum Nancy Shushu wote kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Wengine ni Mkurugenzi wa Usalama na Afya Dkt. Jerome Materu kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Meneja wa Maabara, Emmanuel Gwae, Mkuu wa Kituo cha Taifa cha kudhibiti Sumu, Yohana Goshashy, Mkemia daraja la pili, Amina Omary na Mkemia daraja la kwanza, Florida Tumbu wote Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Washiriki wengine ni Ofisa wa Viwango, Miraji Kambangwa na Simon Kidiga kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Wadau hao waliokutanishwa na AGENDA kila mmoja kwa niaba ya taasisi yake alitoa mwelekeo wa kile watakachokitekeleza mara baada ya kikao kazi hicho.
Kwa upande wa AGENDA ikiwakilishwa na Katibu Mtendaji, Dorah Swai ilipendekeza kuwepo kwa muungano wa pamoja wa wadau hao katika kushughulika na rangi zilizo na madini ya risasi.
Pendekezo la pili ni kuwa na kikosi kazi kitakachokuwa na jukumu la kutembelea wazalishaji wa rangi, kuendeleza kampeni za kuwajengea uelewa wananchi na wazalishaji na pia AGENDA iliiomba TBS kuendelea kuwaelimisha wazalishaji wa rangi na ikiwezekana kuwawajisha ili lengo la kuwa na asilimia sifuri ya madini ya risasi kwenye rangi linafikiwa kwa haraka.
Kwa upande wake mwakilishi wa OSHA, Dkt. Materu, pamoja na kuiomba AGENDA kuwapatia matokeo ya vipimo vya vinasaba 38 walivyopima kwenye maabara mbili za Tanzania na moja ya Marekani, aliahidi taasisi yake kuendelea kusimamia sheria.
Aidha NEMC, TBS na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, nao kwa pamoja waliomba kupatiwa matokeo ya vipimo hivyo ili kuyafanyia kazi kwa haraka.
Katika kuhitimisha kikao kazi hicho kilichofunguliwa na Ofisa Program Mkuu wa mwakilishi wa Asasi ya AGENDA, Silvan Mng’anya, Bi. Dorah aliahidi kuwasilisha taarifa za matokeo hayo kwa taasisi hizo.
“Tuko tayari kuwapatia hizi taarifa na ikiwezekana tualikeni ili tukutane na viongozi wa taasisi zenu ili tuone namna bora zaidi ya kufikia asilimia sifuri ya madini ya risasi kwenye rangi.”amesema.
MADINI YA RISASI KWENYE RANGI YANAINGIAJE KATIKA MIILI YA WATOTO?
Kwa ujumla watoto hawako katika hatari ya madini ya risasi (risasi) katika rangi wakati rangi hiyo ikiwa bado katika kiwekeo chake (mfano kopo) au wakati rangi ikiwa ndiyo kwanza imepakwa katika sehemu ambayo haikuwahi kupakwa.
Risasi inakuwa na madhara pale inapokuwa imeshapakwa kwenye ukuta, sakafu, mdoli au sehemu nyingine.
Baada ya muda kupita, rangi huanza kumenyeka, kuchakaa na kuharibika. Risasi iliyoko katika rangi huingia katika vumbi na udongo katika maeneo ya ndani na yanayozunguka makazi, shule na sehemu za kuchezea watoto.
Watoto wanaocheza kwenye maeneo hayo hupata vumbi au udongo kwenye mikono yao na kumeza risasi kutokana na tabia yao ya kutia mikono kinywani.
Watoto wenye umri wa miaka sita na chini ya umri huo wapo katika hatari zaidi kwani kundi hili la watoto linaathirika zaidi kutokana na risasi.
Utafiti wa kisayansi uliofanyika mwaka 2014 na kuchapishwa kwenye jarida la Kisayansi inakadiriwa kuwa kwa wastani watoto wenye umri wa kuanzia mwaka mmoja mpaka sita wanameza vumbi na udongo uliopo maeneo ya makazi kwa ] takribani miligramu 100 kwa siku.
MADHARA YA KIAFYA
Ubongo wa mtoto mdogo unakua, huongezeka na kutambua vitu kwa haraka. Risasi huingilia utendaji huo.
Risasi iliyoingia mwilini hata kwa kiwango kidogo, madhara yake hayatibiki, na hudumu kwa maisha yote.
Madhara hayo ni kama ifuatavyo:
Kupunguza uwezo wa kuelewa,
Kuongezeka kwa tabia ya hasira na ukorofi,
Matatizo ya uzazi kwa wanaume, athari hizo huwa kubwa zaidi kulingana na uchanga wa mtoto na mtoto anayetungwa yuko hatarini zaidi.
VIWANGO VYA MADINI YA RISASI KIMATAIFA
Kwenye miaka ya 1970 na 1980 nchi nyingi zilizoendelea zilipitisha sheria, kanuni au viwango vya kisheria vya risasi katika rangi ili kulinda afya ya watu wake.
Viwango vilivyopitishwa na Marekani viliweka ukomo wa juu wa risasi katika rangi wa sehemu 90 kwa milioni (90 ppm) ya risasi katika rangi kavu, rangi za nyumba na rangi za aina nyingine.
Nchi nyingine zimepitisha viwango vya ukomo kisheria kama vile sehemu 90 au 600 ya milioni ya risasi katika rangi kavu.
MADHARA YA KIUCHUMI
Kupungua uwezo wa uelewa kunasababisha madhara kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.
Utafiti uliofanyika ulionyesha kuwa gharama ya jumla ya Dola za Marekani, US$977 bilioni zinatumika kwa mwaka katika nchi zenye uchumi mdogo na wa kati kutokana na madhara ya risasi.
Utafiti huo umekadiria upotevu wa US$134.7 bilioni kila mwaka barani Afrika, au 4% ya pato la taifa.
MLINDE MTOTO
Ili kumlinda mtoto na athari za madini ya risasi kwenye rangi, ulizia rangi ambayo haijaongezwa risasi.
Kampuni duniani zimekuwa zikizalisha rangi bila kuongeza risasi kwa miaka mingi na aina nyingi ya rangi zinazoongoza katika soko hazina risasi.
Safisha nyumba kwa kutumia maji hasa katika maeneo ya madirisha na milango maeneo ambayo ni rahisi rangi kumenyeka na kusambaa.
Hamasisha wauza rangi katika masoko ya ndani kuuza zile tu ambazo hazijaongezwa risasi.
Unga mkono juhudi za kuzuia kiwango cha risasi katika rangi kisizidi sehemu 90 ya milioni (90 ppm).
Tangu madini ya risasi yaondolewe katika mafuta ya petrol, madini ya risasi katika rangi yamekuwa mojawapo ya vyanzo vya risasi kwa watoto.
Rangi zenye risasi bado zinatumika katika nchi nyingi. Zaidi ya hayo, rangi zenye risasi zinaweza kuwa chanzo cha risasi na madhara ya kiafya kwa miaka mingi baada ya rangi kupakwa katika eneo.
Uhusiano kati ya risasi katika rangi na madhara yake kwa afya ya watoto na watu wazima walioingiwa na risasi katika miili yao umethibitishwa kikamilifu.
Kadri rangi inavyochakaa kulingana na muda, watoto wanaweza kuvuta au kumeza risasi kupitia vumbi la nyumbani, vipande vya rangi au udongo uliochafuliwa na risasi.
Watoto waliopata madhara ya kiafya kutokana na risasi watakuwa na madhara hayo kwa maisha yao yote.
