Featured Kitaifa

WAZIRI MKUU AWASIMAMISHA MAOFISA WANNE WA TRA MUTUKULA

Written by mzalendoeditor

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi kwenye Kituo cha Huduma za Pamoja cha Mutukula, wakati alipotembelea kituo hicho, Septemba 23, 2023. Mheshimiwa Majaliwa yupo mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua miundombinu katika kituo cha afya cha Kakunyu kilichopo Missenyi, Mkoani Kagera, Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa. Kituo hicho kimegharimu shilingi milioni 500

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi wakati alipokagua miundombinu katika kituo cha afya cha Kakunyu. Mheshimiwa Majaliwa yupo mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi

Muonekano wa Kituo cha Afya Kakunyu ambacho Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kuona maendeleo ya ujenzi wake

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia shehena ya mizigo inayoshushwa kwenye Lori kwa ajili ya kukaguliwa kabla haijavushwa kwenda nchi jirani, wakati alipotembelea Kituo cha Huduma za Pamoja cha Mutukula ili kuona utendaji kazi wake

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua shughuli mbalimbali katika Kituo cha Huduma za Pamoja cha Mutukula alipotembelea kituo hicho, Septemba 23, 2023. Mheshimiwa Majaliwa yupo mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Afisa Forodha wa Uganda, Joseph Kamulegeya, wakati alipokagua shughuli mbalimbali katika Kituo cha Huduma za Pamoja cha Mutukula alipotembelea kituo hicho, Septemba 23, 2023. Mheshimiwa Majaliwa yupo mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi 

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi kwenye Kituo cha Huduma za Pamoja cha Mutukula, wakati alipotembelea kituo hicho, Septemba 23, 2023. Mheshimiwa Majaliwa yupo mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 

 

 …..…………..

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) cha Mutukula, Bw. Feisal Nassoro na wenzake watatu warudishwe makao makuu mara moja na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Watumishi wengine ni Bw. Gerald Mabula, Bw. George Mwakitalu na Bw. Emmanuel Malima ambao ni maafisa mapato wa TRA.

Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Septemba 23, 2023) wakati akizungumza na wafanyabiashara na wakazi wa Mutukula mara ya kufanya ukaguzi kwenye Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani (One Stop Border Post) cha Mutukula, wilayani Missenyi mkoani Kagera.

“Watumishi hawa wanne warudishwe makao makuu kwa sababu ya kudharau mamlaka na kuikosesha Serikali mapato. Ukaguzi ulifanywa na Kamati ya Usalama ya Wilaya wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya lakini walipewa dharau kana kwamba hiki ni chombo kilicho juu ya sheria.”

“Mkuu wa Wilaya ni mkuu na msimamizi wa shughuli za Serikali ndani ya wilaya yake. Anapotaka taarifa anastahili apatiwe. Uongozi wa mkoa ulipokuja nao pia waliambulia dharau. Hatuwezi kukubali kuona mtumishi wa umma anafanya mambo ya hovyo halafu sisi tunamuacha,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye ziara ya mikoa ya Kusini alisisitiza kuwa mtumishi ambaye hatekelezi majukumu yake, sisi hatutamvumilia. “Ni lazima watumishi tuwe na nidhamu ya kazi, ni lazima tuheshimu mamlaka,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wakazi wa Mutukula wachangamkie fursa ya uwepo wao mpakani na kuimarisha biashara zao.

“Mutukula ni mji wa kibiashara na unakua kwa kasi sana. Hapa Mutukula ni sawa na Tunduma, Kasumulo, Sirari na Namanga. Lazima mji huu uwe unakimbiliwa na watu wa nje na wa ndani. Hivyo Halmashauri ya Wilaya ijipange ijenge kituo kizuri cha mabasi ili watu wakija wapate mahali pa kupumzikia.”

Waziri Mkuu yuko mkoani Kagera kwa ziara ya siku tatu. 

 

About the author

mzalendoeditor