Featured Kitaifa

SERIKALI YAWEKA MIKAKATI YA KUONDOA FOLENI YA MAROLI -TUNDUMA

Written by mzalendoeditor

 

Na Mwandishi wetu – Songwe 
 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara amewahakikishia wadau wanaotumia kituo cha forodha Tunduma kuvusha mizigo kupitia Nakonde upande wa Zambia kuwa kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zambia Mheshimiwa Hakainde Hichelema kwamba watendaji wahakikishe kuwa changangamoto zote zinazowakabili wasafirishaji mizigo kwenda nchi za Zambia DRC Zimbabwe na nchi nyingine zinatafutiwa ufumbuzi wa haraka.
 
Prof. Kahyarara ameyasema hayo kwenye kikao kilichowakutanisha watendaji wa Serikali wanaofanya kazi katika Mpaka wa Tunduma, “Tayari taasisi ya Trade Mark East Afrika pamoja na Benki ya Dunia wako tayari kugharamia mpango kabambe wa maboresho mradi utakao gharimu dola milioni 27 na kutekelezwa kwa mwaka mmoja” alisema Kahyarara.

 

 

Mradi huo utakapokamilika utawezesha kituo hicho kuwa na mifumo inayosomana kwa kuwa na scanner za kisasa na kutumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA, hatua itakayoongeza ufanisi na ushindani kwa Bandari ya Dar es Salaam. Hatua hii ni baadhi ya mageuzi makubwa yanayotekelezwa na Mheshimiwa Rais Dr Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuimarisha bandari na kukuza biashara na uchumi.

 

 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Francis Michael amesema kuwa pamoja na mkakati wa kuongeza upana wa barabara katika eneo hilo lakini bado kila mtu anayefanya kazi katika enao hilo ahakikishe anatimiza wajibu wake ili kuondoa msongamano wa Maroli.
 
Pia Dkt. Francis amesema kuwa Mkoa huo umejipanga kuanza kujenga bandari kavu eneo la Tunduma ili kuweza kupaki magari yote ambayo anasubilia kuvuka mpaka kwenda nchi jirani.
 
Naye Kamanda wa Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe SSP Joseph Bukombe amesema kuwa kwasasa wameweka utaratibu wa kuvusha magari kwa awamu ili kupunguza foleni katika mpaka huo.
 
Mpaka wa Tunduma na Nakonde unakadiliwa kuvusha maroli zaidi ya elfu moja mia mbili kwa siku kutoka Tanzania kwenda Zambia, DRC Congo na Zimbabwe.

About the author

mzalendoeditor