Na.Suzan Alex-MZALENDO BLOG-DODOMA
MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeandaa jukwaa la majadiliano linalowakutanisha Asasi za Kiraia (CSOs), mawakili pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo Wizara ya Katiba na Sheria na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kwa lengo la kujadili masuala ya haki za binadamu na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wote.
Jukwaa hilo linalenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu sera, sheria na changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa haki, pamoja na kujadili namna bora ya kuzitatua na kuweka mikakati ya kufanya maboresho katika mifumo ya kisheria nchini.
Akizungumza leo Novemba 24, 2026, jijini Dodoma, Mkuu wa Idara ya Utetezi wa THRDC, Wakili Paul Kisabo, amesema jukwaa hilo ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali, Asasi za Kiraia na mawakili ili kuhakikisha jamii inapata haki na usawa.
Amesema kupitia mjumuiko huo, wadau hao wataweza kuunganisha nguvu katika kutoa elimu ya haki za binadamu kwa umma na kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na changamoto za kisheria.
“Tunaamini kupitia mjumuiko huu wa mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na mawakili na Serikali, kwa pamoja tutaweza kufikisha elimu kwa umma, kuwasaidia watu wenye changamoto za kisheria pamoja na kuleta maendeleo,” amesema Kisabo.
Ameongeza kuwa jukwaa hilo pia limelenga kujengeana uelewa, kujadili changamoto zilizopo katika sekta ya haki za binadamu na kuimarisha ushirikiano baina ya wadau ili kupata suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Sheria kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Andrew Samanyi, amesema jukwaa hilo ni muhimu kwa kuwa litasaidia kuimarisha mahusiano na ushirikiano kati ya Serikali na Asasi za Kiraia katika kushughulikia masuala ya kisheria yanayowagusa wananchi.
Amesema Asasi za Kiraia zina nafasi kubwa katika kuibua changamoto zinazowakabili wananchi kuanzia ngazi ya chini kupitia tafiti na shughuli mbalimbali wanazozifanya, hivyo ushirikiano wao na Serikali unaweza kusaidia kupata suluhisho la changamoto hizo.
“Tunaamini CSOs zinaangazia kuanzia chini ambako zinapata mambo mengi kupitia tafiti zao, ambazo kwa namna moja au nyingine zinashirikiana na Serikali kuona namna gani zinaweza kutatua changamoto za wananchi pamoja na kuangalia sheria zipi zinatakiwa kufanyiwa maboresho ili kujenga ustawi wa jamii na wananchi kwa ujumla,” amesema Samanyi.
Amesisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na Asasi za Kiraia ni nyenzo muhimu katika kubaini mapungufu yaliyopo katika sheria na mifumo ya utoaji haki, pamoja na kupendekeza maboresho yatakayochochea ustawi wa jamii.


