Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo,akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 28,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) imeweka mikakati kabambe ya kuimarisha usimamizi, ukaguzi na uendeshaji wa vyama vya ushirika nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha sekta hiyo inakuwa imara, yenye uwazi na inayochangia kikamilifu uchumi wa wananchi.
Hayo yamesemwa leo Aprili 28, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali itafanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vyama vya ushirika 6,545, huku COASCO ikikagua vitabu vya hesabu vya vyama hivyo vyote vilivyosajiliwa katika mfumo wa MUVU ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji unaimarika.
Aidha, Maafisa Ushirika 80 watapatiwa mafunzo maalum ya usimamizi wa vyama vya ushirika, huku Maafisa wengine 60 wakipatiwa vitendea kazi ikiwemo kompyuta na pikipiki 60 ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Katika kuboresha utendaji, Tume itatoa mafunzo ya utunzaji wa kumbukumbu na uandaaji wa vitabu vya hesabu kwa vyama vyote 6,545, hatua inayolenga kuhakikisha vinazingatia sheria na taratibu za uendeshaji.
Kwa upande mwingine, Serikali itatathmini na kuzipanga upya taasisi 4,894 za ushirika wa mazao kulingana na uwezo na mali zao, ili kubaini aina sahihi ya usimamizi unaohitajika kwa kila chama.
Aidha, kampeni maalum ya “Linda Ushirika Chagua Uadilifu” itazinduliwa kwa lengo la kuelimisha wadau mbalimbali ikiwemo mahakama, polisi, TAKUKURU na wanasheria kuhusu uadilifu, usimamizi bora na utatuzi wa migogoro ndani ya vyama vya ushirika.
Katika kuongeza nguvu ya kiuchumi ya vyama hivyo, Serikali kupitia Ushirika Joint Enterprise (UJE) na Benki ya Ushirika Tanzania itaendelea kuhamasisha vyama kuongeza umiliki wa hisa kutoka asilimia 45 hadi 51, pamoja na kuviwezesha vyama vikuu 25 kuwa mawakala wa benki na kufungua matawi katika mikoa mbalimbali nchini.
Katika sekta ya viwanda vya ushirika, Serikali itaendelea kuratibu ujenzi na ufufuaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao, ikiwemo kiwanda cha kubangua korosho cha TANECU Tandahimba, kiwanda cha pamba cha Magu, kiwanda cha mafuta cha KACU Kahama, pamoja na kiwanda cha maziwa CHAWAKIM mkoani Pwani.
Aidha, Chama Kikuu cha Tabora (WETCU) kitaendelea kusimamiwa kujenga kiwanda cha nyuzi za kusukia tumbaku katika kongani ya viwanda vya pamba mkoani Simiyu, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao na ajira.
Serikali pia imeweka mkazo katika kuhamasisha vyama vya ushirika kuuza mazao kupitia mifumo rasmi na jumuishi ya biashara ili kuongeza uwazi, ushindani na mauzo ya ndani na nje ya nchi.
Katika kuimarisha ushirika kwa makundi maalum, Tume itahamasisha uanzishaji wa vyama vya vijana 26 pamoja na vikundi 127 vya wafugaji na wavuvi, ili kuongeza upatikanaji wa mitaji na kuimarisha masoko ya mazao yao.
Vilevile, wakulima wa mazao ya chikichi, viazi mviringo, ngano na tufaha watahamasishwa kujiunga na ushirika, huku mashine 18 za kuongeza thamani ya chikichi zikitarajiwa kusambazwa katika vyama 18.
Kwa upande wa kimataifa, Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Kongamano la Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Barani Afrika (SACCA Congress) Oktoba 2026, tukio litakalolenga kuimarisha ushirika na uwekezaji katika sekta hiyo.