Featured Kitaifa

SAMIA SCHOLARSHIP EXTENDED YAFUNGUA FURSA URUSI KWA WANAFUNZI 10

Written by Alex Sonna

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-Dodoma

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza fursa mpya ya ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 10 wa Kitanzania kwenda kusoma nchini Urusi kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo  Agosti 13, 2026, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema wanafunzi hao wamepata fursa hiyo kutoka Chuo Kikuu cha RUDN kilichopo Moscow, kufuatia ziara rasmi ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi iliyofanyika Juni mwaka huu.

Amesema wanafunzi hao wanatarajiwa kuondoka nchini Septemba Mosi, 2026, kuelekea Moscow, ambako wataanza kambi maalumu ya maandalizi ya masomo (bootcamp) itakayodumu kwa takribani miezi 10 kabla ya kuanza masomo yao ya shahada ya kwanza.

“Katika kipindi cha bootcamp, Serikali ya Urusi itagharamia asilimia 80 ya gharama na Samia Scholarship Extended itagharamia asilimia 20,” amesema  Prof. Mkenda.

Ameongeza kuwa baada ya wanafunzi hao kumaliza kambi hiyo na kuanza masomo rasmi ya shahada ya kwanza, Serikali ya Urusi itagharamia asilimia 100 ya gharama za masomo yao.

Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, wanafunzi hao 10 wanaungana na wanafunzi wengine 50 waliotangazwa awali, hivyo kufanya jumla ya wanafunzi watakaonufaika na mpango huo kufikia 60.

Amesema wanafunzi hao watasomea fani za Data Science, Artificial Intelligence (Akili Unde) na Allied Sciences, ambazo ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayolenga kukidhi mahitaji ya ujuzi wa kisasa na kusaidia Taifa kukabiliana na changamoto za kiteknolojia.

Prof. Mkenda amesema wanafunzi 50 waliopata fursa awali wataanza kambi yao ya mafunzo katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela African Institution of Science and Technology (NM-AIST), Arusha, kuanzia Septemba 14, 2026, huku wakitakiwa kuripoti chuoni hapo Septemba 13.

Akizungumzia mchakato wa uteuzi, Waziri huyo amesema wanafunzi hao walichaguliwa kwa kuzingatia ufaulu wa juu katika mitihani ya Kidato cha Sita, hususan katika michepuo ya sayansi ya PCM, PGM na PMC.

Amesema  wanafunzi 50 waliokuwa katika nafasi za kwanza hadi ya 50 walichaguliwa kwenda Arusha, huku waliokuwa katika nafasi ya 51 hadi 60 wakipata fursa ya kusoma nchini Urusi.

“Kati ya wanafunzi 10 wanaokwenda Urusi, wanafunzi nane wanatoka katika shule za Serikali na wawili wanatoka shule binafsi,” amesema 

Profesa Mkenda amesisitiza kuwa Serikali imezingatia misingi ya uwazi na uadilifu katika mchakato wa uteuzi, ili kuhakikisha fursa hizo zinawanufaisha wanafunzi wenye uwezo unaostahili.

Aidha, amesema  Wizara inaendelea kuratibu maandalizi ya safari ya wanafunzi hao, ikiwamo kuwawezesha kupata pasipoti, ambapo wanafunzi tisa kati yao hawakuwa na pasipoti.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wanafunzi hao wanakamilisha maandalizi yote muhimu na kuondoka nchini kwa wakati kuelekea Moscow.

Profesa Mkenda amefafanua kuwa majina ya wanafunzi wote 10 waliochaguliwa yatawekwa kwenye tovuti rasmi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ili kuwawezesha wananchi kupata taarifa zaidi kuhusu wanufaika wa fursa hiyo.

About the author

Alex Sonna