Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amepokea mwaliko wa kushiriki katika dua maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaombea viongozi wa nchi pamoja na kuliombea Taifa katika kipindi hiki cha matarajio ya mvua zinazohusishwa na hali ya El Niño.

Rais Dkt. Mwinyi amepokea mwaliko huo leo, tarehe 16 Septemba 2026, Ikulu, Zanzibar, alipokutana na uongozi wa Almadrasat Swifat Nabawiyatil Karimah, Msolopa Kilimani.

Uongozi wa madrasa hiyo umeeleza kuwa dua hiyo inatarajiwa kufanyika siku ya Ijumaa, tarehe 18 Septemba 2026, na itajumuisha maombi maalum kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Aidha, dua hiyo imelenga kuliombea Taifa na wananchi wake kutokana na matarajio ya hali ya El Niño na mvua kubwa, sambamba na kumuomba Mwenyezi Mungu aliepushe Taifa na madhara yanayoweza kujitokeza.

Uongozi huo pia umemueleza Rais Dkt. Mwinyi kuwa Maulid ya madrasa hiyo inatarajiwa kufanyika tarehe 19 Septemba 2026, ikiwa ni sehemu ya shughuli za kidini zilizoandaliwa na taasisi hiyo.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameridhia ombi la viongozi wa madrasa la kuongeza nafasi za Hijja kutoka tatu za mwaka jana hadi sita mwaka huu, sambamba na kuwashukuru kwa mwaliko na maandalizi ya dua maalum ya kuwaombea viongozi na Taifa.

Amesema ni jambo la faraja kuona taasisi za dini zikiendelea kuwa sehemu ya kuombea amani, ustawi na maendeleo ya nchi, pamoja na kuwahimiza wananchi kumuomba Mwenyezi Mungu katika vipindi mbalimbali vinavyohitaji mshikamano wa kijamii na kiroho.

Naye, Amir Mkuu wa Madrasat Swifat Nabawiyatil Karimah, Alhaj, Sheikh Muhammad Salum Muhammed, amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa kupokea mwaliko huo na kwa kukubali ombi la nafasi sita za Hijja, akieleza kuwa hatua hiyo imepokelewa kwa shukrani kubwa na uongozi wa madrasa.