Featured Kitaifa

TARURA WAPATIWA MAFUNZO YA MATUMIZI YA TAARIFA ZA HALI YA HEWA

Written by Alex Sonna

Na Mwandishi Wetu – Dodoma

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imepatiwa mafunzo kuhusu matumizi ya taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara za wilaya nchini.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo kwa watendaji wa TARURA, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a amesema ni muhimu usanifu na utekelezaji wa miundombinu ya barabara kuzingatia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka hiyo.

Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watendaji wa TARURA kutumia taarifa za hali ya hewa hususan utabiri wa msimu wa mvua ili kuwezesha kuchukua tahadhari mapema na kupanga kwa ufanisi shughuli za ujenzi na matengenezo ya barabara.

Dkt. Chang’a amesema matumizi sahihi ya taarifa hizo yatasaidia kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa na kuongeza ufanisi na uimara wa miundombinu ya barabara nchini.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff ameishukuru TMA kwa kutoa mafunzo hayo, amesema elimu hiyo itawawezesha watendaji wa Wakala kutumia taarifa za hali ya hewa katika usanifu, ujenzi na matengenezo ya barabara za wilaya nchini.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya miundombinu inatekelezwa kwa kuzingatia mabadiliko na mwenendo wa hali ya hewa nchini.

About the author

Alex Sonna