Na. OWM–TAMISEMI, Dodoma
Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) inaandaa mkakati wa kuboresha miundombinu ya michezo na kuimarisha mafunzo kwa walimu wa michezo shuleni, hatua inayolenga kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kuwawezesha kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
Hayo yamebainishwa leo, Agosti 13, 2026, jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Sera na Mipango OWM–TAMISEMI, Bw. John Cheyo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, wakati akijibu hoja za wajumbe katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Bw. Cheyo ameeleza kuwa mkakati huo, unaolenga kuimarisha michezo na kukuza vipaji vya wanafunzi, utawasilishwa kwa Kamati hiyo ili kupata maoni na mapendekezo ya maboresho kabla ya kuwasilishwa Wizara ya Mipango kwa ajili ya kupata idhini ya kuanza kutumika.
Aidha, amesema OWM–TAMISEMI, kwa kutambua umuhimu wa michezo katika shule za msingi na sekondari, tayari imeunda Kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo chenye jukumu la kusimamia na kuratibu maendeleo ya michezo katika shule hizo nchini.
Sanjari na hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo OWM–TAMISEMI, Bw. Yusuph Singo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, amewasilisha kwa Kamati hiyo mkakati wa Serikali wa kujenga viwanja vya michezo 368 na kuboresha viwanja 920 katika shule za msingi 1,000 na sekondari 288.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kila shule inakuwa na angalau kiwanja kimoja cha michezo kinachokidhi viwango stahiki kwa ajili ya utekelezaji wa Somo la Elimu ya Viungo na Michezo, pamoja na kutoa mazingira bora ya wanafunzi kuibua na kuendeleza vipaji vyao.
Bw. Singo amesema Serikali pia ina mkakati wa kuongeza idadi ya walimu wenye taaluma ya Elimu ya Viungo na Michezo kwa kuajiri na kuwajengea uwezo walimu wapya 2,000, ambao watapangwa katika shule zenye uhitaji mkubwa kwa lengo la kuboresha uwiano wa walimu na shule.
Aidha, amesisitiza kuwa OWM–TAMISEMI itaendelea kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika kutoa mafunzo kwa walimu wa michezo nchini kupitia Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.
Akitoa maelekezo ya Kamati, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Florent Kyombo, ameitaka Serikali kuwa na mkakati madhubuti wa kuzalisha walimu wa michezo katika shule za msingi na sekondari, sambamba na kuwa na mkakati madhubuti wa kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi ili taifa liweze kupata wanamichezo wenye uwezo wa kuliwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
Kikao hicho kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na watendaji wa OWM–TAMISEMI, kilichojadili mkakati wa ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya michezo katika shule za msingi na sekondari pamoja na ajira za walimu wa michezo, ni sehemu ya maandalizi kuelekea Mkutano wa Nne wa Bunge unaotarajiwa kuanza Agosti 25, 2026.
