Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo,akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 28,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Wizara ya Kilimo imeliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha jumla ya Shilingi trilioni 1,105,950,115,000 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za sekta ya kilimo katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Hayo yamesemwa leo Aprili 28, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema fedha hizo zinalenga kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuendeleza huduma muhimu za kilimo, pamoja na kugharamia matumizi ya kawaida ya Wizara, Bodi na taasisi zake.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, katika Fungu 43 pekee, Wizara imeomba jumla ya Shilingi 698,985,584,000 ambapo sehemu kubwa ya fedha hizo zitatumika katika miradi ya maendeleo.
Kati ya fedha za maendeleo, Shilingi 567,345,730,000 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati, ambapo Shilingi 360,678,811,000 ni fedha za ndani na Shilingi 206,666,919,000 ni fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Aidha, Shilingi 131,639,854,000 zitatumika kwa matumizi ya kawaida ya Wizara, ambapo Shilingi 84,956,697,000 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi, na Shilingi 46,683,157,000 ni kwa matumizi mengine ya kiutendaji ya Wizara, Bodi na taasisi zake.
Wizara imeeleza kuwa bajeti hiyo inalenga kuimarisha utekelezaji wa programu mbalimbali za kilimo, kuongeza tija kwa wakulima, kuimarisha usalama wa chakula, pamoja na kukuza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa taifa.