Zaidi ya watu 30 wanadaiwa kufariki dunia katika ajali mbili tofauti zilizotokea usiku wa kuamkia leo mkoani Morogoro, huku wengine 37 wakinusurika na askari wa Jeshi la Polisi wakitajwa kuwa miongoni mwa wanaodaiwa kupoteza maisha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amethibitisha kutokea kwa Ajali hizo.
Amesema ajali ya kwanza imetokea eneo la Miti Bora katikati ya maeneo ya Dakawa na Dumila wilayani Mvomero, majira ya saa moja kasoro robo usiku wa Oktoba 08 mwaka huu likihusisha gari iliyokuwa na askari na gari nyingine ambapo watu wanne wamefariki Dunia.
Ajali ya pili imetokea eneo la Mkambarani, Kikombe cha chai, majira ya saa nne na nusu usiku wa Oktoba 08 mwaka huu, katika Wilaya ya Morogoro ambako magari mawili likiwemo basi la abiria likitokea Dar es salaam kwenda Iringa liligongana uso kwa uso na Lori lililokuwa limebeba Mbao likitokea uelekeo wa Morogoro kwenda uelekeo wa Dar es salaam na kuwaka moto
Katika ajali hiyo basi la abiria limeteketea kwa moto, huku idadi kubwa ya watu ikihofiwa kuathirika ikiwemo vifo na majeruhi.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Joseph Mwasabeja, amesema jeshi hilo lilifanikiwa kukamilisha zoezi la kupata miili ya marehemu na kusaidia kuwafikisha majeruhi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.
“Awali tulitoa gari Moja liende eneo la tukio lakini tukaambiwa Ajali hiyo sio nyepesi kama tunavyodhani, tukaongeza magari mengine mawili, kufika Hali ilikuwa mbaya, tayari moto ulikuwa umeshika kila sehemu, tumepambana na moto na hatua yetu kubwa ya kwanza ni kuokoa maisha ya watu, na baadaye Mali, lakini kulingana na mazingira wakati mwingine mnalazimika kwenda na vyote kwa wakati mmoja” Alisema Mwasabeja
Chanzo:Nipashe Digital