Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesisitiza umuhimu wa taasisi za umma kuzingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 pamoja na Kanuni za mwaka 2024, ili kulinda fedha za umma na kuhakikisha wananchi wanapata thamani halisi ya miradi na huduma zinazotekelezwa.
Akifungua mafunzo jijini Mwanza, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Fatuma Mganga, amesema kila shilingi ya mlipakodi inapaswa kutumika kwa ufanisi na kuleta matokeo yanayolingana na thamani ya mradi au huduma husika.
Kwa upande wake, Afisa Sheria wa PPRA, Fikiri Ngakonda, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea watendaji uelewa kuhusu mabadiliko katika sheria na kanuni mpya, pamoja na matumizi sahihi ya mfumo wa NeST katika hatua mbalimbali za ununuzi wa umma.
Afisa ununuzi na ugavi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Amina Kamenya, amesema mafunzo hayo yaliyoandaliwa na PPRA yatawaongezea uwezo maafisa ununuzi kutambua na kupata watoa huduma wanaokidhi vigezo kupitia mfumo wa NeST, hatua itakayosaidia kupunguza makosa na hasara katika matumizi ya fedha za serikali
Naye mkuu wa sehemu ya huduma za sheria katika Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma, PPAA, Agnes Sayi, amesema PPAA na PPRA zina makubaliano ya kushirikiana katika kutoa elimu kuhusu ununuzi wa umma na kanuni zake
Amesema wataendelea kutoa elimu kuhusu namna ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko pamoja na rufaa katika michakato ya zabuni za umma, ili kuwawezesha wadau kufahamu hatua za kufuata pale wanapoona hawajatendewa haki.
Mafunzo hayo yamewakutanisha zaidi ya washiriki 150, wakiwemo maafisa ununuzi na ugavi, wanasheria na viongozi wa taasisi mbalimbali, kwa lengo la kuongeza uelewa, kuimarisha uwazi na uwajibikaji na kupunguza makosa katika matumizi ya fedha za umma.
