Na.Mwandishi Wetu- Dodoma
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake na kuitaka kuharakisha matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS) katika zao la parachichi ili kuongeza tija kwa wakulima.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Deodatus Mwanyika, ametoa pongezi hizo leo Agosti 20, 2026 jijini Dodoma baada ya Kamati hiyo kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya WRRB kwa mwaka 2025/26.
Mhe. Mwanyika amesema Kamati imeridhishwa na utendaji kazi wa WRRB, hasa katika kushughulikia changamoto za wananchi, na kuitaka Bodi hiyo iongeze kasi katika utoaji elimu ili kuchochea matumizi ya mfumo huo katika maeneo mengine.
Akitoa ufafanuzi wa hoja za wajumbe, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, ameahidi kufanyia kazi maelekezo ya Kamati hiyo na kuihakikishia kuwa ataendelea kulinda majukumu ya taasisi zilizo chini yake kwa mujibu wa sheria.
Awali, akiwasilisha taarifa kwa Kamati hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, amesema kwa mwaka 2025/26, WRRB imetoa leseni kwa waendesha ghala 235, kusajili ghala 951, wanunuzi 390, waweka mali 2,667 na kutoa stakabadhi za ghala 214,170.
