Na.Mwandishi Wetu-DODOMA
CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimekabidhi vifaa vya kisasa vya upimaji wa afya ya Mama Mjamzito vinavyotumia teknolojia ya akili unde (AI) ultrasound kwa vituo 32 vya kutolea huduma za afya mkoani Dodoma, vyenye thamani ya shilingi milioni 352.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa leo Septemba 15, 2026, katika kituo cha afya Mkonze, jijini Dodoma, kupitia Mradi wa safari, unaolenga kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto kwa kutumia teknolojia, pamoja na kuongeza uwezo wa wahudumu wa afya katika kufanya uchunguzi wa wajawazito.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema uwepo wa vifaa hivyo katika vituo vya afya utaongeza uwezo wa kutoa huduma bora za uchunguzi na kupunguza ulazima wa wajawazito kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Amesema teknolojia hiyo itasaidia kufanya uchunguzi wa awali katika vituo vya afya, huku wajawazito watakaogundulika kuwa na viashiria vya changamoto au matatizo wakipewa rufaa kwa wakati kwenda vituo vya ngazi ya juu vyenye wataalamu na wabobezi zaidi kwa ajili ya uchunguzi wa kina na matibabu.
“Vifaa hivi vitatumika kama chombo cha awali katika vituo vyetu vya afya. mama mjamzito atakayegundulika kuwa na viashiria vya changamoto au matatizo yoyote wakati wa uchunguzi, atapewa rufaa haraka kwenda vituo vya ngazi ya juu vyenye wataalamu na wabobezi zaidi wa ultrasound kwa ajili ya uchunguzi wa kina na matibabu,” Amesema Senyamule.
Aidha, Senyamule amewataka waganga wa halmashauri zote nane za mkoa wa Dodoma pamoja na watumishi wa vituo vya afya vitakavyokabidhiwa vifaa hivyo kuvitunza na kuvitumia kwa usahihi, ili viweze kutoa matokeo yaliyokusudiwa na kuendelea kuimarisha huduma kwa wananchi.
kwa upande wake, Mkurugenzi wa shahada ya uzamili kutoka UDOM, Profesa Josephat Kiligiti, amesema mradi huo unalenga kujifunza namna teknolojia ya akili unde (AI) inavyoweza kuunganishwa na huduma za kawaida za afya ya mama na mtoto, hasa katika ngazi ya msingi.
“Ni muhimu kutambua kwamba changamoto ya upungufu wa wataalamu wa ultra sound sio tatizo la Dodoma pekee bali ni tatizo la kitaifa na hata kimataifa katika nchi nyingi zinazoendelea, teknolojia hii inaweza kuziba pengo hilo,”amesema.
Naye Naibu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Nasoro Mzee ametoa rai kwa Wakuu wa Wilaya watakao kabidhiwa vifaa hivyo kuhakikisha vinatumika ipasavyo na sio kwenda kuvifungia stoo.
Awali Mtafiti Mkuu wa Mradi huo Dkt. Leonard Katalambula emesisitiza kuwa teknolojia hiyo haichukui nafasi ya mtoa huduma wala mtaalamu bali ni chombo kinachomsaidia mtoa huduma kufanya uchunguzi na kufanya maamuzi kwa wakati kwa kuzingatia taratibu za kitaalamu.
