Featured Kitaifa

MAKANDARASI WATAKIWA KUFANYIA KAZI MAAGIZO WANAYOPEWA KABLA MVUA ZA EL NINO

Written by Alex Sonna

Dar es Salaam

Makandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara za kuingia viwanja vya mazoezi na uendelezaji wa barabara ya uwanja wa Taifa ambayo itatumika wakati wa michuano ya AFCON wametakiwa kufanyia kazi maelekezo yote wanayopatiwa na Wakala ya Barabara za Vijini na Mijini (TARURA) kabla ya kuanza kwa mvua za El Nino.

Msisitizo huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TARURA Mhandisi Florian Kabaka wakati wa ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa barabara hizo jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Kabaka amesema kwamba Makandarasi hawapaswi kuzungumza tu bali kutekeleza kwa kufanyia kazi yale yote wanayoshauriwa na kuelekezwa na Wakala huo ili mvua zitakavyoanza kunyesha iwakute wamemaliza ujenzi wa mitaro ya maji na hivyo kuepusha maeneo muhimu kutokupata changamoto za maji na kuathiri miundombinu mingine.

Aidha, Mwenyekiti huyo amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi unaoendelea na kuwapongeza kwa kufanya kazi usiku na mchana, pia kuwepo kwa wataalam, mitambo na vifaa vingine inatoa matumaini ya kufikia hatua nzuri hadi kufikia mwisho wa mwezi huu.

Amesema miradi yote inayotekelewa Dar es Salaam imefikia 50% na kuwasisitiza kuongeza kasi zaidi.

Pamoja na hayo, Mhandisi Kabaka aliwatoa hofu wananchi kwamba TARURA watahakikisha wanaboresha barabara zote muhimu wakati wa El Nino ili wananchi wasikwame katika kupata huduma muhimu.

Naye, Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff amesema miradi hiyo inaendelea vizuri na wao kama wasimamizi wataendelea kuwafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha kazi zinamalizika kwa wakati ifikapo Desemba mwaka huu.

Pia amesema kwa hatua iliyofikiwa ana uhakika barabara zote zitakamilika kwa viwango na kufikiwa masharti yaliyowekwa.

About the author

Alex Sonna