Featured Michezo

RAIS WA BARCELONA LAPOTRA ATUMA SALAM ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA MWENZA WA RAIS SAMIA

Written by Alex Sonna

Na Mwandishi wetu – MAELEZO

Rais wa Klabu ya Barcelona FC, Joan Lapotra amemkabidhi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda barua maalum ya rambirambi kwa ajili ya kumfikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia kifo cha mume wake, Mzee Hafidh Ameir Hassan, kilichotokea tarehe 7 Septemba 2026.

Mhe. Makonda amekabidhiwa rambirambi hiyo Septemba 14, 2026, nchini Hispania ambapo amekwenda kwa ziara maalum.

Wakati akikabidhi barua ya rambirambi, rais Lapotra amemtaka Rais Samia kuwa na subira, moyo wa ujasiri na nguvu katika kipindi hicho cha majonzi.

Mhe. Paul Makonda ameanza ziara maalum katika Klabu ya FC Barcelona nchini Hispania yenye lengo la kuangazia fursa za ushirikiano zitakazochochea maendeleo ya soka la Tanzania.

Ziara hiyo ya siku nne iliyoanza tarehe 14 hadi 17 Septemba, 2026 ni kufuatia mwaliko wa Rais wa klabu hiyo, Joan Laporta.

Waziri Makonda ameanza ziara hiyo kwa kutembelea timu ya Barcelona na kufanya mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo yaliyojikita katika maeneo ya kukuza vipaji, maendeleo ya kiufundi, uendeshaji wa timu ya taifa.

Vilevile, wamejadili namna uzoefu wa Barcelona unavyoweza kusaidia maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Pia, Mhe. Makonda anatarajiwa kushuhudia mchezo kati ya Barcelona na Racing Santander utakaochezwa tarehe 16 Septemba 2026 katika Uwanja wa Camp Nou, jijini Barcelona.

Katika ziara hiyo, Mhe. Makonda ameambatana na wataalamu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Barcelona inatambulika duniani kwa mfumo wake wa kukuza na kuendeleza vipaji vya wachezaji, jambo linaloifanya kuwa miongoni mwa klabu zinazotumika kama mfano katika maendeleo ya soka la kisasa.

Aidha, sehemu kubwa ya wachezaji wa timu ya taifa ya Hispania iliyotwaa Kombe la Dunia 2026 wametokea FC Barcelona.

About the author

Alex Sonna