Featured Kitaifa

PROF. SHEMDOE AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA MADARASA LINDI

Written by Alex Sonna
Na: OWM – TAMISEMI, Mchinga – Lindi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa madarasa manne na ofisi moja ya Mkuu wa Shule ya Msingi Mkwajuni, Kata ya Kitomanga, Manispaa ya Lindi, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo yake ya kuhakikisha shule hiyo inarejeshewa miundombinu iliyoharibiwa na maafa.
Shule hiyo ilikumbwa na maafa Januari 29, 2026, ambapo madarasa mawili, ofisi ya Mwalimu Mkuu, nyumba mbili za walimu na vyoo vya wanafunzi viliezuliwa, huku darasa moja likiangukiwa na mkorosho.
Prof. Shemdoe ameweka jiwe la msingi katika mradi huo Septemba 14, 2026, alipofika shuleni hapo kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa hayo na ofisi ya Mkuu wa Shule, unaogharimu Shilingi Milioni 96. Ujenzi huo ulianza baada ya hoja iliyowasilishwa Bungeni na Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mhe. Salma Rashid Kikwete, akiomba Serikali kutoa usaidizi wa haraka kufuatia maafa yaliyolikumba shule hiyo.
Kufuatia hoja hiyo, Prof. Shemdoe alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi kuhakikisha fedha zinapatikana kwa haraka kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hayo manne, agizo ambalo lilitekelezwa.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Prof. Shemdoe amesema Serikali imeonesha utayari wa kuchukua hatua za haraka pale wananchi wanapokabiliwa na changamoto zinazohitaji suluhisho la dharura.
“Mhe. Mkuu wa Mkoa, tuliomba ridhaa kwa Mhe. Rais ya kuomba fedha za kujenga madarasa haya manne ziletwe mara moja, na leo hii wote tumeshuhudia madarasa manne mazuri pamoja na ofisi ya Mkuu wa Shule hii ya Mkwajuni yaliyotokana na juhudi za Mbunge Mhe. Salma Rashid Kikwete za kuomba usaidizi wa haraka,” amesema Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amewahakikishia wananchi wa Kata ya Kitomanga kuwa OWM–TAMISEMI italeta fedha nyingine kwa ajili ya kujenga madarasa zaidi katika shule hiyo, ili hatimaye shule hiyo iwe na madarasa mapya na kuondokana na matumizi ya madarasa ya zamani yaliyopo katika hifadhi ya barabara.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mhe. Salma Rashid Kikwete, amemshukuru Prof. Shemdoe kwa kuweka jiwe la msingi katika katika Shule ya Msingi Mkwajuni, huku akimuomba kuendelea kusaidia upatikanaji wa majengo mengine ya madarasa na ofisi ili walimu wapate mazingira bora zaidi ya kufanyia kazi na wanafunzi kujifunza katika mazingira salama na rafiki.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Adam Kighoma Malima, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kumuamini na kumpa jukumu la kusimamia upatikanaji wa maendeleo kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi.
Mhe. Malima pia amemshukuru Mhe. Rais kwa utayari wake wa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akiahidi kuendelea kuwatumikia wananchi wa Lindi kwa bidii na moyo wa uzalendo.
Katika ziara yake mkoani Lindi Septemba 14, 2026, Prof. Shemdoe pia ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo Mradi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko; Mradi wa ujenzi wa Jengo la Wazazi (Maternity Ward) na Jengo la Wodi ya Matibabu ya Watoto Wachanga (NCU) katika Hospitali ya Wilaya ya Kinyonga; Mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi katika eneo la Sekondari Mkunyule, Kata ya Mandawa; pamoja na Mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Kitomanga ‘B’.

About the author

Alex Sonna