Featured Kitaifa

BALOZI SALUM AZITAKA FCC, TBS NA WMA KUPAMBANA NA BIDHAA BANDIA NA DUNI.

Written by Alex Sonna

 

Mameneja wa Kanda na Mikoa wa Taasisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Tume ya Ushindani (FCC) pamoja na Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) wameagizwa kuhakikisha hakuna bidhaa bandia na duni katika maeneo yao wanayoyasimamia kiutendaji.

Maelekezo hayo yametolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Balozi Waziri Rajab Salum, wakati wa kikao cha menejimenti za Tume ya Ushindani (FCC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Agosti 21, 2026 jijini Dodoma, kwa lengo la kujadili na kupanga mikakati ya kuimarisha udhibiti wa bidhaa bandia nchini.

Katika kikao hicho, Balozi Salum amesisitiza umuhimu wa taasisi hizo kufanya kazi kwa ushirikiano, weledi, haki na uwajibikaji, akieleza kuwa uratibu mzuri ni muhimu katika kuhakikisha bidhaa zisizokidhi viwango na bidhaa bandia hazitawali soko.

Amesema udhibiti wa bidhaa bandia ni suala muhimu katika kulinda mlaji, wafanyabiashara wanaofuata sheria pamoja na uchumi wa nchi, hivyo taasisi zenye dhamana ya kusimamia soko zinapaswa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Balozi Salum amezitaka FCC, TBS na WMA kuongeza ushirikiano katika kubadilishana taarifa, kufanya ukaguzi na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wanaojihusisha na uzalishaji, uingizaji au usambazaji wa bidhaa bandia na zisizokidhi viwango.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa watumishi wa taasisi hizo kuwa waadilifu na kutekeleza majukumu yao kwa haki, ili kuhakikisha wafanyabiashara wanafuata sheria wanapata mazingira sawa ya ushindani na walaji wanapata bidhaa salama na zenye ubora.

Amesema matumizi ya teknolojia na taarifa sahihi yanapaswa kupewa kipaumbele katika kuimarisha mifumo ya udhibiti, kutokana na mabadiliko ya mbinu zinazotumiwa na baadhi ya watu katika kusambaza bidhaa bandia katika masoko.

Kwa upande mwingine, kikao hicho kimekuwa fursa kwa viongozi wa FCC, TBS na WMA kueleza changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao, pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuongeza ufanisi katika usimamizi wa soko.

Balozi Salum amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi zake ili kujenga mazingira ya biashara yenye ushindani wa haki, kulinda walaji na kuhakikisha wafanyabiashara wanaofuata sheria wanaendelea kufanya shughuli zao katika mazingira salama na yenye tija.

Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Viwanda na Biashara kuimarisha uratibu wa taasisi zake na kuhakikisha majukumu ya udhibiti wa soko yanatekelezwa kwa weledi, haki, uwajibikaji na kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.

About the author

Alex Sonna