Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, akimueleza Meneja wa Mikopo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Amani Shabani (kushoto), kuhusu umuhimu wa Benki hiyo kuendelea kuinua wakulima nchini, wakati alipotembelea katika Viwanja vya Dk. John Samwel Malecelaa kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi, zinazotekelezwa katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo 2026, yanayofanyika katika viwanja hivyo, Nzuguni jijini Dodoma. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, ambaye alimuongoza Mhe. Balozi Omar kutembelea Maonesho hayo yenye kauli mbiu ya ‘‘Tambua soko, Ongeza Tija kutekeleza Dira 2050’’.

Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, wakimsikiliza Meneja wa Mikopo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Amani Shabani, akifafanua kuhusu jitihada za benki hiyo katika kuinua wakulima nchini kupitia utoaji wa mikopo, wakati alipotembelea katika Viwanja vya Dk. John Samwel Malecelaa kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi, zinazotekelezwa katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo 2026, yanayofanyika katika viwanja hivyo Nzuguni jijini Dodoma. Maonesho hayo yana kauli mbiu ya ‘‘Tambua soko, Ongeza Tija kutekeleza Dira 2050’’.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imeiagiza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuongeza kasi ya uwekezaji katika miradi ya kilimo yenye tija ili kuchochea uzalishaji, kuongeza ajira na kuharakisha ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, alipotembelea banda la TADB katika Maonesho ya 49 ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Waziri Omar alisema sekta ya kilimo ndiyo mhimili wa maendeleo ya uchumi wa Tanzania, hivyo taasisi za kifedha zina wajibu wa kuendelea kubuni bidhaa na huduma zitakazowawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kupata mitaji kwa urahisi, kuwekeza katika uzalishaji wa kisasa na kuongeza thamani ya mazao yao.
Alisema Serikali imeonyesha dhamira ya dhati ya kuifanya TADB kuwa injini ya maendeleo ya sekta ya kilimo kwa kuongeza mtaji wa benki hiyo kutoka Sh bilioni 60 hadi zaidi ya Sh bilioni 400, hatua ambayo imeongeza uwezo wake wa kuwafikia wadau wengi zaidi wa kilimo na shughuli nyingine za uzalishaji.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unategemea kwa kiwango kikubwa mageuzi ya sekta za uzalishaji, hususan kilimo, mifugo na uvuvi, ambazo zina mchango mkubwa katika uzalishaji wa malighafi, ajira, usalama wa chakula na ukuaji wa uchumi.
“Kilimo kina nafasi ya kipekee katika safari ya maendeleo ya Taifa. Tunahitaji uwekezaji mkubwa zaidi utakaowawezesha wazalishaji kuongeza tija na ushindani wa bidhaa zetu ndani na nje ya nchi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Omar aliwapongeza wajasiriamali na wazalishaji wanaoshiriki katika maonesho hayo kwa kuendelea kuzalisha bidhaa zenye ubora, akibainisha kuwa sasa nguvu zaidi inapaswa kuelekezwa katika upatikanaji wa masoko ya uhakika na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa.
Aidha, aliitaka Wizara ya Kilimo kuendelea kushirikiana kwa karibu na wazalishaji na taasisi za kifedha ili kuweka mazingira yatakayowezesha kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa bidhaa na kuunganisha wazalishaji na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Alisema ushirikiano huo utasaidia kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kuimarisha kipato cha wakulima na kuchangia kwa kiasi kikubwa kufikiwa kwa malengo ya Serikali ya kujenga uchumi shindani unaotegemea uzalishaji wenye tija.