Uncategorized

WATANZANIA WATAKIWA KUTUMIA NeST KUINUA UCHUMI WA TAIFA

Written by Alex Sonna

Watanzania wametakiwa kuhakikisha wanatumia ipasavyo Mfumo wa NeST kukamilisha michakato ya ununuzi wa umma ili kuinua jamii kiuchumi na kuhakikisha fedha zote zinazotengwa zinasimamiwa kwa umakini mkubwa na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

Akizungumza katika Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma, lililoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Julai 29, 2026, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila, aliyemwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amesema sekta ya ununuzi wa umma inahusisha sehemu kubwa ya matumizi ya fedha za Serikali, hivyo ni lazima isimamiwe kwa ufanisi na uadilifu.

Ameongeza kuwa matumizi ya Mfumo wa NeST ni matokeo ya ubunifu uliofanywa na Watanzania kwa kuwezeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita, ambao unapaswa kutumika kuchochea uzalishaji na ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira, kuimarisha kampuni za ndani, kukuza ubunifu na kuhakikisha maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha Watanzania wengi zaidi.

“Ununuzi wa umma na ugavi ni nyenzo ya kisera na kimkakati ya Serikali katika kuchochea uzalishaji na ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira, kuimarisha kampuni za ndani, kukuza ubunifu na kuhakikisha maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha Watanzania wengi zaidi,” amesema Dkt. Toba Nguvila.

Amewataka watumishi wa umma kuhakikisha wanazingatia matakwa ya sheria kwa kutofanya ununuzi wa umma nje ya mfumo na kuzingatia upendeleo maalum kwa makundi maalum, wazabuni na bidhaa za ndani ya nchi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba, alieleza kuwa Mamlaka hiyo inazingatia na kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo ni pamoja na kuhakikisha taasisi zote za umma zinafuata sheria na taratibu za ununuzi; kuwataja hadharani viongozi na taasisi zinazokiuka taratibu hizo; kuhakikisha miradi yote inatoa thamani halisi ya fedha zilizotengwa; pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya PPRA, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika kudhibiti rushwa na ubadhirifu.

Katika kongamano hilo, PPRA ilitoa tuzo kwa taasisi zilizofanya vizuri katika ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria na thamani ya fedha kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, matumizi ya Mfumo wa NeST, pamoja na utekelezaji wa takwa la kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa makundi maalum, ambayo ni vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

 

About the author

Alex Sonna