Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia binti mwenye umri wa miaka 16 kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi, Hadija Shaha (51), katika Kijiji cha Msoga, Wilaya ya Chalinze, baada ya kuzuiwa kuhudhuria sherehe ya siku ya kuzaliwa ya rafiki yake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salum Morcase, amesema leo Alhamisi Julai 30, 2026 kuwa tukio hilo lilitokea saa 5:00 usiku wa Julai 28, 2026 katika Kijiji cha Msoga.
Amesema mtuhumiwa, Rahma Tito, anadaiwa kumshambulia mama yake ambaye alikuwa na ulemavu wa miguu yote miwili, kisha kumchoma kichwani kwa kutumia kitu chenye ncha kali.
Kwa mujibu wa Morcase, uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo kuwa ni ugomvi ulioibuka baada ya marehemu kumzuia binti huyo kwenda kwenye sherehe ya siku ya kuzaliwa ya rafiki yake iliyokuwa ikifanyika karibu na Hospitali ya Msoga.
Inadaiwa kuwa baada ya kuzuiwa, binti huyo alianzisha ugomvi ulioishia kwa shambulio lililosababisha kifo cha mama yake.