Uncategorized

CHATANDA: JENGO LA KISASA LA MAKAO MKUU YA CCM  NI URITHI WA DKT.SAMIA

Written by Alex Sonna

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

MWENYEKITI wa  Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda, amepongeza uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa utekelezaji wa ujenzi wa jengo kubwa na la kisasa la Makao Makuu ya chama hicho , akisema  ni sehemu ya urithi wa uongozi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Chatanda ameyasema hayo leo Septemba 24,2026 jijini Dodoma wakati wa ziara ya Viongozi na watendaji wa UWT ngazi ya Wilaya,Mikoa na Taifa kutembelea eneo linalojengwa jengo hilo, ambapo ameeleza kuwa wazo la kuanzisha mradi huo lilitokana na maono ya Dk. Samia na baadaye kuwasilishwa katika vikao mbalimbali vya chama vilivyolijadili na kulipitisha.

Amesema hatua iliyofikiwa katika ujenzi huo inaonyesha dhamira ya CCM ya kuwa na miundombinu ya kisasa itakayokidhi mahitaji ya chama na shughuli mbalimbali, huku akiwapongeza viongozi na watumishi wanaosimamia utekelezaji wa mradi huo.

“Haya ni maono makubwa ambayo ameyafanya, ambayo anakusudia kuacha legacy ya chama chetu. Wazo linaanza na mtu mmoja, lakini baadaye linashirikishwa na viongozi wengine na kufikia hatua ya kuwa utekelezaji wa pamoja,” amesema  Chatanda.

Chatanda pia amewapongeza vijana na watumishi wa CCM kutoka Makao Makuu wanaosimamia mradi huo, akisema wameonyesha uwajibikaji katika kuhakikisha ujenzi unaendelea kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa.

Amesema miongoni mwa mambo yaliyomvutia katika jengo hilo ni uwepo wa ukumbi wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua watu 500, akieleza kuwa miundombinu hiyo itakuwa na umuhimu katika kuendesha shughuli mbalimbali za chama na jumuiya zake.

Aidha amewahimiza wasimamizi kuongeza kasi ya utekelezaji ili kukamilisha mradi kwa wakati na kuwezesha uzinduzi wake kufanyika mwezi Februari wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya CCM.

“Miezi iliyobaki ni michache, lakini tuna matumaini makubwa kwa sababu hatua iliyofikiwa inaonekana mnaweza kuongeza kasi ili mwezi wa pili, tunapoadhimisha miaka 50 ya chama chetu, tuje hapa kwa ajili ya uzinduzi wa jengo hili,” amesema 

Hata hivyo  Chatanda amempongeza Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Asha-Rose Migiro, kwa usimamizi wa utekelezaji wa maazimio ya chama, akisema nafasi yake ni muhimu katika kuhakikisha maamuzi yanayopitishwa na vikao vya chama yanatekelezwa.

Amesema utekelezaji wa mradi huo ni miongoni mwa mifano inayoonyesha uwezo wa wanawake katika uongozi na utekelezaji wa miradi mikubwa, akitumia fursa hiyo kuwataka wanawake kujiamini na kutumia nafasi zao kuleta matokeo katika jamii.

“Wanawake tunaweza. Siku zote tulikuwa tunasema wanawake hawawezi labda wawezeshwe. Sisi tunaweza hata bila kuwezeshwa, na ushahidi ni huu,” amesema Chatanda, huku akimtaja Dk. Samia kuwa mfano wa mwanamke aliyefanya mambo makubwa katika uongozi.

Chatanda alisema ujenzi wa jengo hilo unaonyesha dhamira ya kuacha alama katika historia ya chama, huku akitoa pongezi kwa viongozi wote walioshiriki katika kufanikisha mradi huo na kuwataka wasimamizi kuendelea kuongeza kasi hadi ukamilike.

“Tunamshukuru sana na kumpongeza Mwenyekiti wetu Dk. Samia Suluhu Hassan na kumuombea aendelee kuwa na afya njema. Tumetembelea na tumeona kazi nzuri inayofanyika hapa. Tunawapongeza wote, hususan wasimamizi wa mradi, amesema 

Kwa upande wake Naibu  Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mwanaasha Khamis Juma, amesema wajumbe wa Baraza la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa wameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo la ukumbi wa mikutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema lina viwango na lina vifaa mbalimbali vya kisasa.

Amesema ziara hiyo imewapa wajumbe fursa ya kujionea wenyewe maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo na kupata maelezo kuhusu hatua iliyofikiwa, ambapo kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu wanaosimamia ujenzi, kazi hiyo imefikia takribani asilimia 50.

“Leo tumetembelea jengo hili, ni jengo la ukumbi wa mikutano wa CCM, jengo lenye viwango, kubwa na zuri. Tumeridhika kuona kazi zinaendelea na hatua iliyofikiwa ni nzuri, amesema  Mwanaasha.

Amesema maendeleo hayo yanaonyesha kuwa malengo yaliyowekwa katika utekelezaji wa mradi huo yanaendelea kufikiwa, huku akiwapongeza viongozi wa CCM kwa kuwezesha ujenzi wa jengo hilo ambalo, kwa mujibu wake, lina huduma na miundombinu mbalimbali itakayoongeza uwezo wa chama katika kuendesha shughuli zake.

Mwanaasha pia amewapongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kazi wanazofanya katika kuimarisha chama na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Tunawapongeza viongozi wetu wa chama, Chama Cha Mapinduzi, lakini pia tunapongeza jitihada za chama chetu kwa kutujengea jengo hili. Ni jengo zuri na lina facilities nyingi sana,” amesema 

Aidha, Naibu Spika huyo ameeleza kuvutiwa na ubunifu wa jengo hilo, ikiwemo mpango wa kuwa na eneo la kutua helikopta, akisema ni jambo jipya kwake na linaonyesha kuwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa hakuna kinachoshindikana iwapo dhamira ipo.

Amesema uwepo wa miundombinu hiyo utaifanya CCM kuwa na mazingira bora zaidi ya kuendesha mikutano na shughuli zake, huku akitoa pongezi kwa viongozi na wataalamu wanaosimamia mradi huo kwa kuhakikisha ujenzi unaendelea.

Mwanaasha, amesema wajumbe wamefarijika kuona hatua iliyofikiwa katika ujenzi huo na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazolenga kuimarisha miundombinu na shughuli za chama.

“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa na kushiriki shughuli za UWT kwa siku tatu. Leo tumepata pia nafasi ya kutembelea jengo letu hili na kujionea maendeleo yake. Kwa kweli tunaridhika na tunatoa pongezi kwa uongozi wa chama, amesema 

Awali Msimamizi wa mradi huo, Msanifu Majengo Lucas Martin,amesema kuwa jengo hilo litakuwa la kisasa lenye ghorofa tano pamoja na ukumbi wa kisasa wa mikutano (auditorium) wenye uwezo wa kuchukua takribani watu 500.

Amesema jengo hilo pia litakuwa na ofisi mbalimbali za chama, zikiwemo za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, pamoja na ofisi za watumishi wengine.

“Mpaka sasa, mradi wetu umefikia asilimia 55 na kazi zinazoendelea zaidi ni za ukamilishaji ikiwemo kupiga plaster, kusawazisha kuta (), na kupaka rangi,” amesema Martin

Ameongeza kuwa kazi nyingine zinazoendelea ni ufungaji wa mifumo ya kiyoyozi (AC), mifumo ya kuzima moto, pamoja na mifumo ya TEHAMA.

Amesisitiza kuwa matarajio ni kukamilisha ujenzi huo ifikapo Februari 5, 2027, ikiwa ni siku ambayo CCM itatimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

“Tunatarajia mpaka tarehe hiyo tuwe tumekamilisha ujenzi wa jengo letu kikamilifu,” amesema

About the author

Alex Sonna