Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ( TADB), Frank Nyabundege, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Julai 30, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa benki hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imejipanga kuongeza kasi ya uwekezaji katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kupitia utoaji wa mitaji, matumizi ya teknolojia na ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuchochea uchumi wa Taifa na kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mpango huo umetangazwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege, wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 30,2026 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa shughuli za benki hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na mwelekeo wa mwaka 2026/2027.
Nyabundege amesema TADB imeendelea kutekeleza dhamira yake ya kuwa chachu ya mageuzi ya sekta ya kilimo kwa kuhakikisha wakulima, wafugaji na wavuvi wanapata mitaji inayowawezesha kuongeza uzalishaji, kutumia teknolojia za kisasa na kuingia katika kilimo cha biashara chenye tija.
“Mafanikio ya benki hiyo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo imeendelea kuimarisha mtaji wa TADB na kuongeza uwezo wake wa kuwafikia wananchi wengi zaidi.”amesema Bw.Nyabundege
Bw. Nyabundege, amesema hatua hiyo imeifanya benki kuongeza utoaji wa mikopo kwa kiwango kikubwa, huku asilimia 73.6 ya mikopo yote iliyotolewa katika kipindi cha miaka mitano ikitolewa kuanzia mwaka 2022 hadi 2025.
Amesema pamoja na mtaji unaotolewa na Serikali, TADB imeendelea kuvutia fedha kutoka kwa taasisi za maendeleo za kimataifa, jambo lililoongeza uwezo wa benki kufadhili miradi mikubwa ya uzalishaji na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Nyabundege amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 benki hiyo itaweka nguvu zaidi katika kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa sekta za uzalishaji, kuimarisha minyororo ya thamani ya mazao ya kimkakati, kuongeza mauzo ya bidhaa za kilimo katika masoko ya ndani na nje ya nchi, pamoja na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
Hata hivyo ameongeza kuwa TADB itaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa za kilimo, kufadhili miradi inayokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, na kutoa fursa zaidi za kifedha kwa vijana na wanawake ili washiriki kikamilifu katika uchumi wa kilimo.
“Tunataka kuona kilimo kinakuwa mhimili mkubwa wa ukuaji wa uchumi, kinazalisha ajira nyingi, kinaongeza kipato cha wananchi na kinaifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula na bidhaa za kilimo katika ukanda wa Afrika,” amesema
Aidha, amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo katika kuongeza rasilimali za uwekezaji ili kuhakikisha sekta ya kilimo inachangia kwa kiwango kikubwa zaidi katika maendeleo ya Taifa.
Katika hatua nyingine, Nyabundege amewahimiza wananchi kutembelea banda la TADB katika Maonesho ya 88 ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) mwaka 2026 ili kupata taarifa kuhusu huduma za mikopo, dhamana za kifedha na fursa nyingine zinazotolewa na benki hiyo kwa wadau wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.