Featured Michezo

KARIA ATOA ONYO KALI, TIMU ZINAZOKWEPA VYUMBA VYA KUBADILISHIA NGUO KUNYANG’ANYWA POINTI TANO

Written by Alex Sonna

Na Mwandishi Wetu, Mzalendo blog-Dar es Salaam

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeweka kanuni mpya itakayozitaka klabu zote kutumia vyumba vya kubadilishia nguo vilivyotengwa katika viwanja vya mechi, huku timu yoyote itakayobainika kukiuka utaratibu huo bila sababu za msingi itakabiliwa na adhabu ya kupokwa pointi tano.

Hatua hiyo imelenga kuimarisha nidhamu, uwazi na usimamizi wa mechi za ligi mbalimbali nchini, sambamba na kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya timu kuhusu mazingira ya vyumba hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 30, 2026, katika ofisi za TFF, Rais wa Shirikisho hilo, Wallace Karia, amesema tayari wameandaa vifaa maalumu vitakavyowekwa katika vyumba vya kubadilishia nguo kwa ajili ya kusaidia uchunguzi wa malalamiko yanayowasilishwa na klabu.

Amesema vifaa hivyo vitaiwezesha TFF kupata ushahidi wa moja kwa moja kuhusu hali halisi ya vyumba vya kubadilishia nguo na kuondoa sintofahamu zinazoweza kujitokeza baada ya mechi.

“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa timu kuhusu vyumba vya kubadilishia nguo. Sasa vifaa tulivyonunua vitatumika kufanyia uchunguzi wa madai mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa, ili maamuzi yafanywe kwa haki na kwa kuzingatia ushahidi,” amesema Karia.

Amesisitiza kuwa kuanzia sasa klabu zote zitalazimika kufuata utaratibu uliowekwa wa kutumia vyumba hivyo isipokuwa pale kutakapokuwa na sababu za msingi zitakazokubalika na mamlaka husika.

Kwa mujibu wa Karia, timu itakayokaidi utaratibu huo bila maelezo ya kuridhisha itachukuliwa hatua kali za kinidhamu, ikiwemo kupokwa pointi tano, ikiwa ni sehemu ya juhudi za TFF kuhakikisha kanuni za mashindano zinazingatiwa na kila mshiriki.

About the author

Alex Sonna